Na ELIZABETH JOACHIM – TUDARCO
NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta, amewasili na kujiunga na kambi ya timu hiyo inayojiandaa kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Botswana, utakaochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mchezo huo wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Taifa Stars inahitaji kupata ushindi ili kupanda katika viwango vya ubora vya shirikisho hilo.
Akizungumza jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema mbali na Samatta, mchezaji mwingine wa Stars, Simon Msuva, anayecheza soka nchini Morocco, alitarajiwa kuwasili usiku wa kuamkia leo kujiunga na wenzake.
Alisema kuelekea mchezo huo, maandalizi ya timu yako vyema, ambapo wachezaji wanafanya mazoezi asubuhi na jioni na kabla ya kuanza kwa kambi hiyo madaktari wa Stars waliwafanyia vipimo wachezaji, lakini hakuna aliyeonekana kuwa na tatizo kubwa la kumfanya akose mchezo huo.
Katika hatua nyingine, Alfred alisema timu ya Botswana inatarajia kuwasili Alhamis tayari kuwakabili Stars, ambapo timu hiyo itakuwa na msafara wa watu 27, ikijumuisha wachezaji 18 na viongozi tisa.
“Botswana watafikia kwenye hoteli ya Urban Rose, Ijumaa jioni watafanya mazoezi katika Uwanja wa Uhuru, ambao ndio utatumika kwa ajili ya mchezo huo na maandalizi ya mchezo wote kwa ujumla yanakwenda vyema,” alisema Lucas.