29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

BABA WA MAYWEATHER AMUONYA MCGREGOR

NEW YORK, MAREKANI

BABA wa bingwa wa ngumi duniani, Floyd Mayweather, Mayweather Snr, amemuonya mpinzani wa mwanaye Conor McGregor, kuwa akae mbali na ngumi anaweza kupoteza maisha yake.

McGregor ambaye ni bingwa wa ngumi mchanganyiko, mwishoni mwa wiki iliyopita alichezea kichapo na Mayweather katika kuwania mkanda wa WBC ‘Money Belt’, bondia huyo ilikuwa mara yake ya kwanza kushiriki ngumi za kutumia mikono tu badala ya mchanganyiko.

Pambano hilo la raundi 12, Mayweather mwenye umri wa miaka 40 aliweza kumchapa mpinzani huyo mwenye umri wa miaka 29 katika raundi ya 10 kwa TKO, jambo ambalo liliwashangaza wengi, Mayweather Snr, amedai ni bora McGregor aendelee na ngumi mchanganyiko.

“Wengi waliamini kuwa McGregor angeweza kushinda pambano hilo kutokana na kujigamba kwake, lakini hata wale waliokuwa wanaamini hivyo wamekuwa kimya sasa.

“Kwa kelele zake nilitarajia kumuona akionesha mambo tofauti, lakini hakuweza kufanya hivyo, alikuwa anafanya makosa sana, nadhani alikuwa anahisi kuwa yupo kwenye ngumi mchanganyiko, kuna wakati alikuwa anampiga Mayweather mgongoni, kisogoni kitu ambacho hakitakiwi.

“Naomba niweka wazi kwamba, kama ataendelea kucheza ngumi hizi ipo siku atakuja kuuawa na bondia mwingine, ni bora akaacha mapema au kurudi kwenye mchezo wake wa awali wa ngumi mchanganyiko,” alisema baba wa Mayweather.

Katika pambano hilo, McGregor raia wa nchini Ireland, alivuna kiasi cha pauni milioni 62 ambazo ni zaidi ya bilioni 176 na milioni 590 za Kitanzania, kiasi hicho cha fedha ni kikubwa ambacho hajawahi kukipata katika maisha yake ya ngumi.

Kutokana na kiasi hicho cha fedha alichokipata, McGregor alifanya sherehe mjini Dublin ya kuwashukuru mashabiki wake huku akitumia pauni 77,643, zaidi ya milioni 221 kwa ajili vinywaji vya mashabiki wake.

“Kutoka moyoni, ninawashukuru sana mashabiki zangu, Mayweather hakuwa na nguvu ya kunipiga, lakini anajua kupambana na ndio maana alinishinda, ninampongeza sana kwa ushindi wake na kumaliza mapambano 50 bila ya kupoteza,” alisema McGregor.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles