32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge lageukwa

anne makindaRipoti mbili tofauti za uchunguzi zilizotangazwa na ikulu jana zimemsafisha aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na madini, Eliakim Maswi, huku pia ikiwaondolea hatia mawaziri wanne waliojiuzulu kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ikulu ya Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema ripoti zote mbili za kiuchunguzi zimeonyesha kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja ambao umewatia hatiani Katibu Mkuu huyo pamoja na mawaziri hao wanne waliong’olewa na Bunge bada ya majina yao kutajwa katika kasfa ya Operesheni Tokomeza.

KUHUSU MASWI/MUHONGO

Sefue alisema Maswi, aliyekuwa akichunguzwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Kamati ya Uchunguzi wa Awali ya Mamlaka ya Nidhamu, zote hazikumkuta na hatia.
“Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma haijabaini kuwepo kwa maslahi binafsi katika uamuzi uliofanywa na Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini wa kuruhusu fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kutolewa.
“Hawakubaini ukiukwaji wowote wa maadili ya viongozi wa umma uliofanywa na Eliakim Maswi. Waliona kuwa yote aliyoyafanya yalizingatia matakwa ya sheria, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na ridhaa ya Tanesco,” alisema Balozi Sefue.
Aliendelea kusema:
“Kamati haijabaini kosa lolote ambalo linaweza kusababisha Eliakim Chacha Maswi, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, kufunguliwa mashtaka ya kinidhamu kwa kukiuka Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 ikisomwa pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 kwa kuruhusu Benki Kuu ya Tanzania kutoa fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow.”
Alisema ushahidi wa vielelezo uliotolewa kwenye Sekretarieti ya Maadili na kwenye Kamati ya Uchunguzi wa awali umejitosheleza kuthibitisha kwambaMaswi alitenda kazi yake kwa kiwango kinachoridhisha kwa kufanya mawasiliano na mamlaka mbalimbali na kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuhakikisha na kujiridhisha kwamba kufungwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow kunafanyika kwa usahihi.
Zaidi alisema hakuna ushahidi wowote kuwa Maswi alikuwa miongoni mwa waliopata mgawo wa fedha au fadhila yoyote kutokana na kufungwa Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kutokana na hali hiyo, alisema mchakato wa kinidhamu, kimaadili na kijinai dhidi yake umefikia mwisho na mwenye mamlaka ya uteuzi atatafakari na kuamua cha kufanya kuhusu ajira yake baadaye.
Balozi Sefue pia alisema aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo hana hatia, kwani wakati wa kumchunguza Maswi pia naye alikuwa akichunguzwa.
“Wakati tunamchunguza Maswi tulikuwa tunamchunguza Profesa Muhongo. Ndiyo maana kuna baadhi walipelekwa kwenye Baraza la Maadili kuhojiwa, lakini yeye hakupelekwa,” alisema Sefue.
Kauli ya Kafulila
Akizungumza kwa njia simu akiwa jijini Arusha, Mbunge wa Kigoma Kusini, ambaye ndiye muasisi wa sakata la Escrow ndani ya Bunge, alisema uamuzi huo ulitarajiwa.
“Uamuzi wa Ikulu kumsafisha Maswi na Profesa Muhongo ulitarajiwa kwa sababu ninao ushahidi wa barua unaoonyesha Ikulu kuhusika katika sakata hili na ndiyo sababu Rais kuvuta miguu,” alisema Kafulila.
Kafulila, ambaye hivi karibuni alipewa tuzo na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaounganisha asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu (THIRD-Coalition), alisema ametimiza wajibu na kwamba atawasilisha hoja kwa viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa hatua zaidi.
“Naamini ‘scandal’ ya Escrow itaiondoa CCM madarakani kama Goldenburg ilivyoiondoa KANU madarakani na mhusika alikuwa huyo huyo…” alisema Kafulila.

Operesheni Tokomeza
Kuhusu Operesheni Tokomeza, ambayo iliundwa kwa ajili ya kupambana na ujangili, Balozi Sefue alisema mawaziri waliojiuzulu kwa sakata hilo hawana hatia kwa kuwa waliwajibika kisiasa tu.
“Tume imejiridhisha kuwa mawaziri wote waliojiuzulu, yaani Dk. Emmanuel Nchimbi, Balozi Khamis Kagasheki, Dk. Mathayo David, Shamsi Vuai Nahodha, hawakuhusika moja kwa moja na makosa yoyote ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza,” alisema Sefue.
Tume ya kuchunguza sakata hilo iliundwa na Rais Jakaya Kikwete Mei, 2014, kufuatia malalamiko ya utekelezaji wa operesheni hiyo kwamba ilikiuka haki za binadamu.
Hata hivyo, alisema Tume imebaini kuwa katika utekelezaji wa Operesheni kulikuwa na matukio ya ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea.
“Ukiukwaji huu umesababisha madhara kwa wananchi mbalimbali, ikiwemo vifo, madhara ya mwili na mengine mengi,” alisema Sefue.
Kwa mujibu wa Sefue, Tume imebaini kuwako kwa ushahidi, ukiwamo ule wa kitabibu dhidi ya watu waliouawa pamoja na waliojeruhiwa wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo.
Alisema Tume ilichunguza matukio 15 ya vifo na kuridhika kuwa vifo tisa kati ya hivyo vilisababishwa na mateso, ambapo watendaji kwenye Operesheni walitumia nguvu kubwa kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa wakati wa ukamataji au kuhoji.
“Kabla ya vifo watu hao walikuwa chini ya ulinzi wa askari wa Operesheni na kuna ushahidi wa kitabibu (medical reports), ushahidi wa kimazingira na ushahidi wa kuona, unaohusisha vifo vya marehemu hao na mateso kutoka kwa askari wa Operesheni,” alisema Sefue.
Mbali na hayo, alisema Tume hiyo iligundua pamoja na mambo mengine, kukamatwa kwa meno ya 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya ngiri 11, mikia ya wanyama mbalimbali 36, ngozi za wanyama mbalimbali 21, pembe za swala 46.
Nyingine ni kukamatwa kwa mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 waliokuwa wanachungwa ndani ya hifadhi na misitu, baiskeli 58, pikipiki 8 na magari 9.
“Katika kipindi cha Operesheni kulikamatwa jumla ya bunduki za kijeshi 18, bunduki za kiraia 1,579, risasi 1,964, mbao vipande 27,913, mkaa magunia 1,242, magogo 858 na misumeno 60.
Alisema hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na mashauri mengine nane (8) ya mauaji ambayo upelelezi wake haujakamilika.
“Hatua za kisheria na kiutawala zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliothibitika kuwatesa watu 15 wakati wa Operesheni, lakini pia hatua za kiuchunguzi zinazofanywa na Takukuru kuhusu tuhuma za rushwa na udanganyifu zilizothibitika zitaendelea,” alisema Sefue.
Aliongeza kuwa silaha zinazodaiwa kumilikiwa kihalali zitafanyiwa uhakiki na ukaguzi wa kina kuhusu umiliki na matumizi yake na endapo hakutakuwa na sababu nyingine za kisheria za kuzuia urejeshwaji, wamiliki warejeshewe silaha zao kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Mali ambazo zimethibitika kuchukuliwa wakati wa Operesheni kwa tuhuma za kuhusishwa na uvunaji haramu wa mazao ya misitu zirejeshwe endapo hakutakuwa na sababu za kisheria kuendelea kuzishikilia,” alisema Sefue.
Alisema Serikali itafanya uhakiki wa vijiji ambavyo vimesajiliwa na vimo ndani ya hifadhi ili kutatua migogoro ya ardhi kati ya hifadhi na vijiji na kuongeza kuwa itahakikisha kunakuwa na ushirikiano wa karibu kati ya Msajili wa vijiji au mamlaka husika na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuepuka kusajili vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi.
Alisema Wizara ya Maliasili na Utalii itatayarisha kanuni zitakazoweka utaratibu wa kuwaondoa watu waliovamia na kujenga makazi katika hifadhi.
“Lakini Sheria zote zinazolinda maeneo ya hifadhi zitafanyiwa marekebisho ili kuongeza adhabu kwa kosa la kuingiza mifugo kwenye Hifadhi bila kujali uraia wa wamiliki wa mifugo hiyo,” alisema Sefue.
Sefue alisema Operesheni ilifanikiwa kupunguza kasi ya mauaji ya tembo kutoka tembo wawili kwa siku hadi tembo wawili kwa mwezi wakati wa Operesheni.
Alisema baada ya kusitishwa kwa Operesheni mwezi Novemba mwaka 2013, wafugaji wengi wamerudisha mifugo yao katika maeneo ya hifadhi, yaani Mapori ya Akiba, Hifadhi za Taifa, Hifadhi za Misitu na Maeneo Oevu na ujangili ukaanza kurejea.
“Watuhumiwa waliokuwa wametoroka kukimbia Operesheni, wameanza kurejea kwenye makazi yao na kuendelea na Vitendo vya Ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles