29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

UPELELEZI KESI YA KITILYA PASUA KICHWA

PATRICIA KIMELEMETA NA MANENO SELANYIKA

UPELELEZI wa kesi inayowakabili aliyekua Kamishna Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili umechukuwa mwaka mmoja na miezi minne sasa ukiwa bado haujakamilika.

 

Katika kesi yao iliyosikilizwa jana kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi bado unaendelea kwa sababu unahusisha nyaraka kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.

 

Wakili wa Jamhuri, Christopher Msigwa, aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

 

Alidai Serikali haijalala katika kufuatilia suala hilo mpaka sasa bado wanaendelea kuwakumbusha wahusika kwa sababu suala lenyewe linahusisha nyaraka kutoka nje ya mipaka ya nchi.

 

Wakili Msigwa aliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

 

Katika kesi hiyo, upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Majura Magafu na Hakimu Mkeha. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 8 mwaka huu itakapotajwa kwa mara nyingine.

 

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mwanasheria wa Benki ya Stanbick, Sioi Solomon pamoja na Miss Tanzania wa mwaka 1996, Shose Sinare.

 

Awali, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

 

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi mwaka 2013 na Septemba mwaka  2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 550  kwa  Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard Charter ya Uingereza.

 

Inadaiwa kuwa Agosti 2 mwaka 2012, Sinare akiwa Makao Makuu ya Benki ya Stanbic yaliyopo Kinondoni, kwa nia ya kudanganya aliandaa nyaraka ya mapendekezo akijaribu kuonyesha kuwa Benki ya Standard ya nchini Uingereza ikishirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania kutoa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni  550 kwa Serikali  ya Tanzania kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa si kweli.

 

Pia siku hiyo hiyo Sinare alitoa nyaraka za uongo za mapendekezo ya kuonyesha kuwa Benki ya Standard ya nchini Uingereza ikishirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania, watatoa mkopo wa Dola za Kimarekani  milioni 550 na kuziwasilisha katika Ofisi za Wizara ya Fedha wakati akijua kuwa si kweli.

 

Anadaiwa kuwa Septemba 20, mwaka  2012 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic nchini yaliyopo Kinondoni, alitenda kosa la kughushi barua.

 

Sinare anadaiwa kughushi barua ya mapendekezo ikionyesha kuwa Benki ya Standard ya nchini Uingereza  ikishirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania, watatoa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 550 kwa Serikali  ya Tanzania  kama ada ya uwezeshaji wa asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa si kweli.

 

Inadaiwa kwamba, Agosti 21  mwaka 2012,  Sinare kwa lengo la kulaghai,  aliwasilisha nyaraka hizo za uongo kuiwezesha Serikali ya Tanzania kupata mkopo huo wa kiasi hicho cha ada ya uwezeshaji, katika Ofisi za Wizara ya Fedha.

 

Washtakiwa hao kwa pamoja  wanadaiwa kughushi nyaraka za makubaliano Novemba 5 mwaka 2012 katika Benki ya Stanbic Makao Makuu Kinondoni kwa nia ya kudanganya, pia walighushi waraka wa makubaliano wa Novemba 5, mwaka 2012.

 

Inadaiwa kuwa waraka huo ulikusudia kuonesha kwamba Stanbic Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors  (Egma) Limited, kuwezesha upatikanaji wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 550 kwa ajili ya Serikali ya Tanzania.

 

Wanadaiwa Machi mwaka 2013 jijini Dar es Salaam, walijipatia Dola za Marekani milioni sita, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo  na zililipwa kupitia  Kampuni ya Egma T Ltd.

 

Washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani milioni sita katika akaunti tofauti tofauti  za benki.

 

Kati ya Machi mwaka 2013 na Septemba mwaka 2015, wanadaiwa  kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles