25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

WANANCHI WATAKIWA KUWAFICHUA WAHAMIAJI HARAMU

Na RENATHA KIPAKA-KYERWA

WANANCHI wilayani Kyerwa, Mkoa wa Kagera, wametakiwa kuacha tabia ya kuishi na wahamiaji haramu na badala yake watoe taarifa katika vyombo vya dola ili hatua zichukuliwe.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Kanali Msataafu Shabani Lissu, wakati alipokuwa akizungumza na MTANZANIA wilayani humo.

Alisema kwamba, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwatumia wahamiaji hao kwa shughuli za kilimo kuanzia miaka ya 70 na kwamba tabia hiyo haiwezi kukubaliwa kwa kuwa kila raia wa kigeni anatakiwa kuishi nchini kwa kufuata utaratibu.

“Wilaya yangu ina zaidi ya wahamiaji haramu 16,000 na wapo katika makundi matatu. Yaani, wapo walioingia nchini mwaka 1970 na kurudi nyuma, wapo walioingia nchini kuanzia mwaka 1994 na wapo walioingia baada ya hapo wanaendelea kuingia.

 

“Kwa kuwa tunajua wapo nchini, mwaka jana tulianza harakati za kuwarudisha kwao ambapo kuanzia Septemba mwaka jana, tumewakamata wahamiaji haramu 270 wakiwa kwenye mashamba ya watu.

 

“Tuliwakamata Warundi 107, waliokuwa wanatoka DRC ni 62, Wanyarwanda walikuwa 62 na waliokuwa wanatoka nchini Uganda walikuwa ni 39.

 

“Pamoja na kuwakamata wahamiaji hao, tuliwakamata pia watu waliokuwa wakiwatunza majumbani kwao na kuwafikisha mahakamani kwa sababu kufanya hivyo walikuwa wakikiuka sheria za nchi.

 

“Kwa hiyo, nawaomba wananchi wasiwapokee na kuwahifadhi wahamiaji hao kwani tukija kwako tukawakuta, ujue utahusika na uvunjaji wa sheria za nchi,” alisema Kanali Lissu.

Katika maelezo yake, mkuu huyo wa wilaya aliyataja baadhi ya maeneo yenye wahamiaji wengi, kuwa ni Isingiro, Murongo, Mabira na Kwenda.

 

“Narudia tena, wananchi pamoja na viongozi wa vitongoji hadi kata, wawafichue wahamiaji hao ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles