Na DEOGRATIAS MUSHI
– JOHANNESBURG
UMOJA wa Afrika (AU) na taasisi mbalimbali za kikanda, wanapaswa kuunganisha juhudi zao ili kupunguza au kumaliza migongano inayozikumba baadhi ya nchi barani humo.
Akizungumza jijini hapa jana, wakati wa kongamano la uongozi barani Afrika, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alisema ubinafsi wa baadhi ya viongozi barani Afrika umesababisha matatizo makubwa yaliyosababisha vifo vya watu, huku wengine wakilazimishwa kuwa wakimbizi.
“Viongozi wetu kwa sasa wanapaswa kuwa makini na kuunganisha juhudi zao ili kuhakikisha kuwa nchi za Kiafrika zinakuwa na hali ya amani na usalama, itakayowasaidia wananchi kushughulikia maendeleo katika nchi zao.
Kwa mujibu wa Rais Mkapa, kama viongozi wa Afrika hawawezi kuzungumza kwa sauti na lengo moja, migogoro itaendelea kuzikumba nchi nyingi na hivyo kuweka maisha ya watu katika matatizo makubwa, kama ilivyo kwa sasa huko Sudan Kusini, Somalia, Libya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC).
Mapema akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna ya kutatua migogoro barani Afrika, Mkapa alishauri kwamba baadhi ya nchi zinapaswa kujifunza kutoka Tanzania, ambayo imekuwa ikikabidhi madaraka kwa amani kutoka utawala mmoja kwenda mwingine bila fujo na migogoro.
“Mwalimu Julius Nyerere aiachia madaraka ya kuwa rais kwa miaka 23 japo watu wengi walitaka bado aendelee, lakini yeye akawaambia hata baada ya Nyerere, Tanzania ni lazima iendelee mbele, na kauli hiyo imefuatwa na marais Ali Hassan Mwinyi, mimi na pia Jakaya Kikwete” alisema Mkapa.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alisema pamoja na juhudi nyingi za kumaliza matatizo yanayoikumba Libya, mauaji bado yanaendelea kwa vile hakuna utawala wa sheria, kwani vikundi mbalimbali vinajichukulia madaraka ya kuongoza nchi hiyo.
Mkutano huo wa siku mbili ambao unahudhuriwa pia na marais wastaafu Olusegun Obasanjo (Nigeria), Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Mohasmed Marzouki (Tunisia), Hassan Mohamud (Somalia) na Mwanasheria Mkuu wa Uganda, Bart Katureebe, unazungumzia umuhimu wa usalama na amani katika kujenga Bara la Afrika lenye maendeleo dhabiti.