Na Walter Mguluchuma
– Katavi
SERIKALI imewaonya Watanzania wapya waliokuwa raia wa Burundi wakatakaobainika kujihusisha na uhalifu ikiwamo kufanya mazoezi ya kivita, ujangili, ubaguzi wa kikabila na dini kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kurejeshwa kwao.
Onyo hilo lilitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwa Watanzania hao wapya wanaoishi katika makazi ya Katumba.
“Wapo baadhi yenu ambao mmeshakubaliwa na kupewa uraia wa nchi hii, zipo taarifa kuwa mnajihusisha na uhalifu ukiwamo ujangili katika hifadhi, pia mna ubaguzi wa kikabila ambapo mnawahamasisha wenzenu wasinunue bidhaa kwenye maduka ya wafanyabiashara wazawa hii haiwezi kukubalika.
“Wenyewe kwa wenyewe mnabaguana kwamba wengine mnatoka milimani na wengine chini ya milima mkidharauliana kwamba upande mmoja ni bora kuliko mwingine, huu si utamaduni wetu Watanzania,” alisisitiza.
Aidha, waziri huyo aliwataka raia hao wapya kuwa wazalendo huku akisisitiza kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kuwapatia uraia ambapo mpaka sasa kuna vyeti vya uraia vipatavyo 7,551 ambavyo havijachukuliwa licha ya wakimbizi walioomba kukubaliwa.
Alisema Serikali haiwezi kuondoa utaratibu wa watu kuingia kwenye makazi hayo bila mtu kuwa na kibali mpaka hapo itakapokuwa imejiridhisha kuwa watu wanaoishi kwenye maeneo hayo watakuwa wameacha vitendo vya uhalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Raphael Muhuga, aliwataka wakimbizi wanaoishi katika kambi hiyo ya Katumba ambao wanataka kurejea Burundi, wawe huru kwani milango iko wazi, jambo la muhimu wazingatie utaratibu.
Aidha, Muhuga aliwataka raia hao kuendelea kutunza mazingira kama ambavyo walivyokuwa wakiyatunza kabla ya kuwa raia rasmi.
Wakati huo huo raia hao wamemuomba Mwigulu kuyafuta baadhi ya madhebu ya dini yaliyopo katika makazi hayo ambayo yanachochea ubaguzi wa dini.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Yusuf Shaabani alimweleza Waziri Nchemba kuwa ubaguzi wa dini umekithiri kwenye makazi yao, ambapo hata kuoana waumini wa madhehebu tofauti wanakataliwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Makazi ya Wakimbizi ya Katumba, Athuman Ingwe, alieleza kuwa makazi ya Katumba yalianzishwa mwaka 1973 na yana watu 78,201 kwa sasa, huku raia wapya wakiwa ni asilimia 98 na waliobaki bado ni wakimbizi wa Burundi.