SEOUL, KOREA KUSINI
MAREKANI na Korea Kusini wanafanya mazoezi ya kila mwaka ya jeshi, ambayo mara nyingi huighadhibisha Korea Kaskazini licha ya wito wa kutaka yasifanyike.
Wiki iliyopita Korea Kaskazini ilionekana kulegeza kamba baada ya awali kutisha kurusha makombora kwenda kisiwa cha Marekani cha Guam, kusema itafuatilia kwanza nyendo za taifa hilo.
Korea Kaskazini tayari imelaani mazoezi hayo, ikisema hatua hiyo ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto.
China na Urusi mwezi uliopita zilipendekeza kusitishwa mazoezi ya kijeshi ili nayo Korea Kaskazini iache kuyafanyia majaribio makombora.
Marekani inasema kuwa mazoezi hayo yatawahusisha wanajeshi wake 17,500 na yatadumu kwa kipindi cha siku 10.
Taifa hilo na Korea Kusini hufanya mazoezi ya kijeshi mara mbili kwa mwaka yanayowashirikisha idadi kubwa ya wanajeshi na zana za kivita.
Mazoezi hayo hujumuisha askari wa ardhini, baharini na angani na hujumuisha mafunzo jinsi ya kukabiliana na ugaidi na mashambulizi ya kemikali.
Pia wakati mwingine hushirikisha wanajeshi kutoka nchi washirika. Mwaka uliopita nchi nyingine tisa zilijiunga nayo.