25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

DIMBA MUSIC CONCERT

Tukio la kubwa la muziki litakalokumbusha 1979

 

MIONGONI mwa matukio makubwa yaliyowahi kutikisa anga ya muziki wa dansi nchini ni uzinduzi wa iliyokuwa Bendi ya Orctestrav Safari Sound wakati huo ikitambulisha mtindo mpya wa Masantula ngoma ya Mpwita.

Tukio hilo lilifanyika katika ukumbi maarufu enzi hizo uliokuwa ukiitwa Safari Resort uliokuwa Kimara jijini Dar es Salaam.

Kikumbi Mwanza Mpango maarufu kama King Kiki ambaye mashabiki wanamtambua zaidi kupitia wimbo wake wa Kitambaa Cheupe ndiye aliyekuwa mwenyeji siku hiyo, akiliongoza Kundi la Wana OSS likiwa na sura za wanamuziki maarufu enzi hizo kama Sammy Makassa, Monga Staniel, Mohamed Twahir na wengine kadhaa.

Miongoni mwa mambo yasiyosahaulika katika tukio hilo ni pale walengwa wenyewe yaani King Kiki na wacheza shoo wake akiwemo Ngalusha Tahisndaa kushindwa kufika jukwaani hadi walipopata msaada wa polisi.

Hatimaye tukio jingine na aina hiyo linatarajiwa kufanyika Septemba 2, mwaka huu katika Ukumbi wa Traverntine uliopo Magomeni, ambapo wanamuziki karibu wote mashuhuri nchini wataunda bendi itakayoumana na bendi kongwe ya Msondo Ngoma Music Band.

Yafuatayo ni majina ya wanamuziki waliothibitisha kushiriki tukio hilo.

 

Kikumbi Mwanza Mpango (King Kiki)

Ni kiongozi wa Bendi ya Wazee Sugu La Capital, ambaye umaarufu wake ulianza tangu mwishoni mwa miaka ya 60, lakini baadaye alitoweka na kuibuka tena mwaka 1977 akiwa na Bendi ya Marquiz Du Zaire, ambapo pia aliasisi mtindo wa Kamanyola Bila Jasho.

Mtindo huo ulikuwa sambamba na nyimbo kama vile Nasema Sina Ndugu, Nimepigwa Ngwala, Mokiki, Ndoa na Mama Kadji na nyingine kibao.

Kiki alifanikiwa zaidi pale alipoihama bendi hiyo na kujiunga na OSS ambapo mtindo wake mpya katika bendi hiyo aliouita Masantula Ngoma ya Mpwita uliweza kuwakamata mashabiki wa ndani na nje ya nchi.

Nyimbo kama Haruna Kaka, Tucheze Masantula, Mama Kabibi, Msimamo wa Nyerere na nyingine kadhaa zilimpa umaarufu mkubwa yeye na bendi yake.

 

Hassan Bitchuka

Huyu ni mwimbaji nguli aliyetinga rasmi Bendi ya NUTA wana Msondo 1973 alipotua tu akawa mwimbaji wa kutegemewa wa sauti ya kwanza na pia mtunzi aliyefanya vizuri kwa tungo zake kama vile Nirudishe Kwetu, Mpenzi Zalina, Aziza na nyingine.

Lakini ukali wake uliendelea kutesa anga la muziki pale alipojiunga na bendi ya Orchestra Mlimani Park akimfuata mwimbaji kipenzi chake Muhidin Maalim Gurumo.

Bitchuka pia aliimba kwa mafanikio akiwa na bendi za OSS na pia bado ni tegemeo katika muziki wa Tanzania ambapo hivi karibuni alitia fora katika onyesho la bendi yake iliyofanya ziara nchini Kenya.

 

Ali Choki

Ukiacha wakongwe pia tamasha hilo litakuwa na wanamuziki wenye umri wa kati akiwemo aliyekuwa mmiliki wa Bendi ya Extra Bongo, Ali Choki au Mzee wa Farasi, ambaye yeye amefanya kazi kubwa akiwa na bendi mbalimbali kama vile Bantu Group, Washirika, African Stars, Extra Bongo, TOT na sasa yupo tena na kundi la Twanga Pepeta.

 

Hussein Jumbe (Mzee wa Kuchechemea)

Ukitaja waimbaji wenye kipaji cha kuimba sauti inayoweza kumfanya msikilizaji ukatokwa na machozi basi ni Hussein Jumbe, ambaye kwa sasa anamiliki Bendi ya Talent.

Lakini kabla ya hapo mkali huyo aliyejiunga na bendi ya Urafiki Jazz mwaka 1984 kisha akachukuliwa na Mlimani mwaka 1986 ametokea kuwa mwimbaji maarufu na pia kuziongoza bendi kubwa ikiwemo Sikinde.

Jumbe pia anafahamika jinsi alivyoshirikiana kwa karibu na wanamuziki kama Gurumo pale alipokuwa Msondo Ngoma, na pia kufanya kazi kwa karibu na Tx Moshi William hasa katika wimbo wa Ajali.

Wanamuziki wengi watakaotumbuiza onyesho hili ni pamoja na mpiga solo hatari Adolf Mbinga, Saad Ally Machine, Chakuku Tumba, Hosea Besi, Juma Kakere, Juma Jerry na wengine kadhaa.

Onyesho hili kwa upande wa wanamuziki hawa waliozungumza na Dimba wamelieleza kama ni historia mpya ambayo haijawahi kutokea katika ardhi ya Tanzania na hivyo inatarajiwa kurudisha uhai wa muziki wa dansi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles