29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MTUMBUIZAJI MAHIRI HUAGA KABLA PAZIA HALIJAFUNGWA

YAWEZEKANA kichwa cha habari hapo juu kikawa kigumu kueleweka kutokana na usemi nilioutumia kama utangulizi wa ninachotaka kukubainishia kwenye ‘Tafakuri Yangu’. Kadiri utakavyoendelea kusoma utauelewa vyema.

Miaka iliyopita filamu zilikuwa zinaangaliwa katika majumba mahsusi ya burudani kama ilivyokuwa tumbuizo na michezo ya kuigiza ya kwenye majukwaani.

Hayakuwa majukwaa ilimradi majukwaa, bali kulikuwa na mapazia mahsusi yaliyokuwa yamefungwa yakizuia mtazamaji asiweze kumuona mtumbuizaji.

Mtumbuizaji akishatajwa mapazia hufunguliwa taratibu katika kuhanikiza vifijo kwa mtumbuizaji anayeanza kukonga nyoyo za mashabiki.

Hicho ndicho kinachoakisiwa na methali niliyotohoa kutoka lugha ya Kiingereza ili kukupa maana sadifu, kwamba mtumbuizaji anayetambua umahiri wake huaga jukwaani na kutoka kabla mapazia ya kuashiria mwisho wa tumbuizo lake hayajafungwa.

Ni usemi unaohusika zaidi kwenye sanaa kwa muktadha wa kubainisha kada za watu mbalimbali wanaofanya vyema kwenye nyanja wanazotumikia.

Ni usemi unaofundisha kwamba usipitilize muda uliotengewa usije kuharibu uzuri wa yote uliyotangulia kuyatenda yaliyokupa sifa.

Basi kama ni mtumbuizaji, Rais John Magufuli anatambua thamani yake kwa maelekezo ya Katiba aliyoapa kuilinda kwa kubainisha wazi kuwa, chapuo analopigiwa la kuongezewa muda wa mihula zaidi ya miwili kuwepo madarakani si sahihi.

Wanaomchapulia wanabainisha kazi njema aliyoifanya hadi sasa kwa muda mfupi aliokaa madarakani, hata kabla hajamaliza muhula wake wa kwanza.

Ametamka takriban juma moja lililopita kuwa hawezi kufanya hicho kinachotakiwa na wanaompigia debe hilo ambalo hakubaliani nalo.

Si tu kwa msingi kuwa kazi yenyewe ya kukaa madarakani ni ngumu, bali kwa kuheshimu Katiba inayoelekeza kipindi cha utawala, inawezekana kazi yake njema ndiyo inashawishi kutamka matakwa hayo kutokana na kukonga nyoyo.

Ieleweke kuwa, ili uweze kutimiza pendekezo la kubadilisha muda wa ukomo wa kutawala uliobainishwa kwenye Katiba, kwanza inahitajika kuifanyia mabadiliko Katiba, kwa kutengua baadhi ya vifungu vinavyoweka ukomo wa muhula. Kazi hiyo si rahisi, ina gharama kubwa za kifedha na kidemokrasia.

Hata kama tumbuizo lake limekonga nyoyo za wengi, wakiwamo wanaotaka aongezewe muda, lakini Rais Magufuli anatambua thamani yake kwa muda mfupi alionao, ndiyo maana katika majibu yake amebainisha kuwa, anajielekeza katika kutumbua majipu yaliyooza ambayo mengine ni hatari na magumu kuyafanyia upasuaji, ni kama jipu tambazi.

Hofu yake ni kuwa, pengine asitokee kiongozi mwingine wa kutumbua kama anavyofanya yeye sasa.

Rais Magufuli anafahamu fika kuwa akikubaliana na yanayohanikizwa kuhusu kuongezewa muda basi wengine watakaotumbuliwa katika kipindi chake wanaweza kutumia kigezo hicho kuotesha majipu mapya na kusababisha mengine yasiyotarajiwa.

Kwa mtazamo wa ‘Tafakuri Yangu’, kinachopaswa kufanyika ni kazi njema anayoifanya kugeuka mfano wa siku za usoni. Kuhakikisha kwamba, madudu anayoyashughulikia hayajirudii, Rais Magufuli hakuingia madarakani na Katiba mpya, bali anatumia misingi iliyokuwapo tangu awali, ikimaanisha kwamba, hata mwingine kabla yake angeweza kufanya kama anavyofanya sasa.

Pengine badala ya kufikiria nyongeza ya muhula kwake, inapaswa kudadisi kwanini haikuwezekana kabla yake? Kama yeye anaweza, wengine walishindwa nini kutimiza anachokifanya sasa kwa nafasi aliyokasimiwa akiwa Rais wa tano.

Bado ‘Tafakuri Yangu’ inakumbuka mchakato mrefu uliotugharimu kutafuta Katiba mpya ambao umekwamia matopeni kukiwa hakuna dalili za kukwamuka.

Sidhani kama tunataka mchakato mwingine wa kubadilisha vifungu vya Katiba, ambao utazusha mabishano na malumbano na pengine hautafikia hitimisho.

Katika hatua hii ya mwanzo, wapo baadhi ya Watanzania wametumia uhuru wao wa kujieleza unaobainishwa na Katiba iliyopo, kutaka nyongeza ya mhula wa kukaa madarakani, ajabu ni kwamba tayari baadhi ya wasiokubaliana na maoni hayo wameanza kutokwa povu kama inavyobainishwa na lugha ya kisasa kuelezea kauli kali zenye kufura hamkani.

Labda kwa watu wa kawaida, lakini kwa mwanasiasa yeyote ambaye yuko katika nafasi ya uongozi wa ngazi yoyote, kwa sasa suala si nyongeza ya mihula, bali mchango wake ni upi katika kazi nzuri anayoifanya Rais Magufuli na utekelezaji wake wa dhima ya kupiga hatua za maendeleo kwenye taifa letu?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles