30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

BODI YA MIKOPO IENDANE NA SERA YA ELIMU KWA WOTE

KATIBA ya Tanzania Ibara ya 13 (2), inatamka wazi kwamba ni marufuku kwa sheria iliyotungwa na mamlaka yoyote nchini kuweka sharti ambalo ni la kibaguzi ama kwa dhahiri au kwa taathira yake.

Sheria hiyo mama imekataza ubaguzi katika nyanja zote, hususan elimu.

Ndiyo maana hatushangai kusikia Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), ana mpango wa kupeleka hoja bungeni kupinga uamuzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kuweka vipengele vinavyowabagua baadhi ya watoto wa Watanzania kupata fursa ya kujiendeleza kielimu.

Wiki iliyopita, Bodi ya Mikopo ilitangaza masharti kumi kwa wanafunzi wanaotarajia kuomba ufadhili kwa mwaka wa masomo 2017/18, huku wale ambao wazazi wao ni wakurugenzi au mameneja waandamizi katika makampuni yanayotambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakikosa sifa mikopo hiyo.

Aidha, watoto wa viongozi na wanasiasa waliosaini fomu za maadili kwa viongozi wa umma, nao wametakiwa kutoomba mikopo kwa dhana kwamba wazazi wao wana uwezo wa kuwalipia ada.

Kuna hoja nyingine kwamba wanafunzi wanaotakiwa kupata mikopo ni wale wasiozidi miaka 30. Bodi ya Mikopo inadai sharti hili limewekwa ili kumpa mkopaji fursa pana ya kuweza kulipa mkopo huo.

Katika kupinga hoja hiyo hapo juu, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Susan Lyimo, aliinukuu sehemu ya Katiba Ibara ya 13 (4) inayosema; ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yeyote.

Akizungumza kuhusu masharti hayo 10 yaliyowekwa na Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wanaotakiwa kukopo, Mdee alisema huo ni ubaguzi wa kielimu ambao ni kinyume na matakwa ya Katiba.

Alisema kuwa walitarajia Serikali itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha watu wake wanapata elimu na hasa mikopo, lakini kwa vigezo hivi, watoto wa madiwani hawataendelea na masomo kwa vile wazazi wao wanaonekana wana mishahara, jambo ambalo si kweli.

Sisi wa MTANZANIA Jumapili tunaamini kuwa wakati umefika kwa HELSB kupitia upya vigezo vya kupata mikopo hiyo ili ikidhi azma yake ya kutoa fursa ya elimu kwa Watanzania wengi.

Tunaamini kigezo cha umri kitawanyima Watanzania wengi kupata mikopo hiyo, ikizingatiwa kuwa baadhi ya wanaonyimwa sasa kwa kigezo hicho, ni wale ambao wazazi wao walishidwa kuwalipia ada kabla Serikali kuja na mpango wa kutoa mikopo.

Serikali itambue kwamba si wanasiasa wote wana uwezo wa kuwalipia ada watoto wao. Haifai kumnyima mtoto mkopo kwa vile tu baba yake ni diwani kwani kimsingi madiwani hawapati mshahara bali posho ya Sh 300,000. Baadhi ya wanasiasa hawa wamepata nafasi hizo kwa umahiri wao wa uongozi na si uwezo wa fedha.

Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, imekuwa ikiahidi kuwatetea wanyonge, hivyo si vyema kumnyima Mtanzania mnyonge fursa ya kupata elimu ya juu kwa kisingizio cha kutokidhi masharti ya mkopo.

MTANZANIA Jumapili tunaungana na wadau wengine wa elimu kuishauri Bodi ya Mikopo ijipange upya ili masharti yake yasije yakawaumiza watoto wa masikini ambao ndio walengwa hasa wa mikopo hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles