Na RACHEL MRISHO – DAR ES SALAAM
JIRANI zetu Kenya juzi wamekamilisha wajibu wao wa kikatiba wa kuwachagua viongozi wao kwa kumpata rais kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8, mwaka huu.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), imemtangaza mgombea wa Muungano wa Jubilee, Uhuru Kenyatta, kuwa mshindi wa nafasi ya urais.
Uhuru amemshinda mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga aliyegombea kupitia muungano wa upinzani wa NASA, ambaye ameshindwa kwa mara ya nne sasa katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.
Siku moja baada ya kutangazwa matokeo hayo, kumeibuka vurugu na maandamano katika maeneo mbalimbali ya Kenya kutoka kwa wafuasi wa Raila na kusababisha polisi kuingilia kati kuyazima.
Maeneo ambayo yametajwa kuhusika na vurugu hizo ni pamoja Mathare, Kisumu, Siaya na Migori.
Inadaiwa kuwa wafuasi hao walifunga barabara na kuchoma moto matairi.
Hoja ya msingi ya waandamanaji hao katika maeneo hayo ambayo ni ngome ya Raila, ni kutokubaliana na matokeo, wakidai kuwa mgombea wao ndiye mshindi halali, si Uhuru kama alivyoptangazwa na IEBC.
Itakumbukwa kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007, baada ya Raila kutangazwa kuwa ameshindwa dhidi ya Mwai Kibaki, yalizuka machafuko makubwa na kusababisha vifo.
Matukio hayo yaliiweka Kenya katika taswira mbaya ambayo si vema kurejea.
Licha ya kutokea vurugu za hapa na pale, ukweli unabaki kuwa Wakenya wameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa katika uchaguzi huo.
Kubwa lililobaki kwao ni kuweza kuvumiliana na kuepuka mihemuko ya kisiasa yenye viashiria vya kuhatarisha amani ya taifa lao.
Wakenya wametoa somo kwa nchi nyingine, hasa za Afrika katika demokrasia, kwa kufanya uchaguzi ambao umeelezwa na waangalizi wa kimataifa kuwa ulikuwa huru na haki kulinganisha na mataifa mengine ambayo yanatumia uchaguzi mkuu kama uwanja wa vita.
Kwa msingi huo, si vibaya Watanzania tukayatazama mambo mema waliyoyafanya jirani zetu na kuyaiga, huku tukizidi kuwaombea wasiingie katika vurugu zitakazolirudisha taifa hilo katika historia mbaya iliyopata kuandikwa mwaka 2007/08.
Ni vema tukawa sambamba na Wakenya kwa namna yoyote ile kusaidia kulinda amani ya Kenya, tukitambua kuwa vurugu hazileti maendeleo bali zinarudisha nyuma uchumi.
Ili ni muhimu tukalitazama kwa jicho la tatu kwa sababu athari za vurugu zitakazotokea licha ya kuiathiri zaidi Kenya, pia zitaigusa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo nchi hiyo ni mwanachama.