26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WAANGALIZI WA KIMATAIFA WASIFU UCHAGUZI KENYA

Wakati upinzani ukipinga matokeo yanayompa Rais Uhuru uongozi, makundi ya waangalizi wa kimataifa yameusifu mchakato wa uchaguzi kuwa ulikuwa huru, wazi na wa haki na ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu kote nchini humo.

Waangalizi hao walisema uchaguzi umepita salama na hakuna visa vya udanganyifu vilivyoshuhudiwa.

Wamewatolea wito Wakenya waendelee kuwa watulivu na kusubiri matokeo rasmi ya uchaguzi.

Aidha kuhusu madai ya upinzani ya kudukua mfumo wa uchaguzi, walisema hilo si jukumu lao kuchunguza.

John Mahama, Rais wa zamani wa Ghana, anayeongoza Tume ya Waangalizi wa Jumuia ya Madola, alisema mfumo wa kupiga na kuhesabu kura ulikuwa wa kuaminika, wa uwazi na hauna shaka.

Aidha jopo la waangalizi wa Umoja wa Ulaya pia limeusifu mfumo wa kupiga kura  na kusema hawajashuhudia kisa chochote cha udanganyifu.

Hata hivyo, kauli zao zinajiri wakati ambapo matokeo ya urais wa uchaguzi huo yanaibua utata, huku upande wa upinzani unaoongozwa na Raila ukidai kuwa mitambo ya tume ya kusimamia uchaguzi ilidukuliwa, madai ambayo tume imeyakana.

Kwenye mkutano na wanahabari jana waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walisema ijapokuwa kulikuwa na changamoto kadha wa kadha ikiwamo kuchelewa kufika kwa vifaa vya kupiga kura katika baadhi ya vituo, utaratibu wa uchaguzi ulikuwa sawa.

Walisema vyombo vilivyohusika vilizingiatia uwazi kabla na baada ya uchaguzi, hivyo kuzingatia demokrasia.

Ujumbe huo umesema baadhi ya mawakala wao kwenye vituo vya kupigia kura waliona mchakato huo ukianza na kukamilika.

Matamshi kama hayo yalitolewa pia na kiongozi wa jopo la waangalizi wa Umoja wa Afrika, Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki.

Jopo hilo lilisema jukumu la waangalizi si kuchunguza uchaguzi ila ni kuangalia utaratibu wake.

Kuhusu madai ya udukuaji wa mitambo ya Tume ya Uchaguzi yaliyoibuliwa na Raila, jopo hilo lilisema tume ndio yenye jibu hilo.

“Sisi si wachunguzi wa Umoja wa Afrika, bali waangalizi wa uchaguzi kama waangalizi wengine,” alisema Mbeki.

Aidha jopo la waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola limeungana na waangalizi wengine kutoa matamshi kama hayo.

Kikundi hicho kimesema  maofisa wake walizunguka katika taifa la Kenya kabla na baada ya uchaguzi na kuridhika na maandalizi yote.

Makundi mengine ambayo yametoa kauli zao ni pamoja na waangalizi kutoka Marekani, wakiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, John Kerry, ambao walisema Wakenya wengi walijitokeza kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa wanashikilia kuwa jukumu la waangalizi wa kimataifa wanapaswa kuvuka mipaka kwa kutoishia mchakato wa uchaguzi bali kufikia kiwango cha kuchunguza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles