NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
TIMU ya Simba imerudisha matumaini ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani baada ya kuwachapa wapinzani wao, Azam FC mabao 2-1 mchezo uliofanyika jana Uwanja wa Taifa jijini hapa.
Simba na Azam zipo kwenye vita kali ya kuwania nafasi ya pili ili kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani, ambapo wekundu hao wameshindwa kukata tiketi ya michuano ya kimataifa toka mwaka juzi waliposhiriki mara ya mwisho.
Azam ambayo mara baada ya mchezo huo imebakiwa na pointi 45 ikiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya Yanga keshokutwa na Mgambo JKT Jumamosi hii, inahitaji pointi tatu tu kwenye mechi hizo zitakazoifanya kufikisha pointi 48 ambazo hazitaweza kufikiwa na Simba.
Simba yenye pointi 44 inabidi iiombee mabaya Azam ipate sare mechi hizo au ifungwe zote, huku na yenyewe ikitakiwa kuifunga JKT Ruvu kwenye mchezo wa mwisho Jumamosi hii ili kupata tiketi ya michuano hiyo.
Wekundu hao walianza kwa kasi mchezo huo na kufanya kosakosa langoni mwa Azam kupitia kiungo, Said Ndemla dakika ya 12 aliyepiga shuti kali la mbali ambalo lilidakwa vema na kipa Aishi Manula.
Azam waliamka dakika ya 14 na kufanya shambulizi kali langoni mwa Simba kupitia kwa Kipre Tchetche, lakini Didier Kavumbagu anakosa bao la wazi akiwa na kipa Ivo Mapunda, baada ya kupiga shuti hafifu lililodakwa kirahisi.
Dakika ya 37, mwamuzi wa kati, Israel Nkongo wa jijini hapa alimuonya kwa kadi ya njano kiungo wa Azam, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa kumchezea madhambi kiungo wa Simba, Jonas Mkude.
Azam ilipata pigo dakika mbili baadaye baada ya Sure Boy kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumfanyia madhambi beki Mohamed Hussein na hivyo kulazimika kucheza pungufu hadi mwisho wa mchezo.
Kabla ya timu zote kwenda mapumziko, ilitokea piga nikupige langoni mwa Simba baada ya kiungo wa Azam, Frank Domayo kuingiza krosi iliyowababatiza mabeki wa Simba na Mapunda alilazimika kufanya kazi ya ziada kuokoa na kufanya kipindi cha kwanza kuisha kwa suluhu.
Azam ilifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kumtoa Domayo na kuingia Bryson Rafael, kisha ikamtoa beki Pascal Serge Wawa na kuingia kiungo Mudathir Yahya.
Simba ilitumia vema mwanya wa Azam kuwa pungufu kwa kupata bao la uongozi dakika ya 48 lililofungwa na mshambuliaji Ibrahim Ajibu akiunganisha vema pasi ya beki Hassan Kessy.
Dakika ya 53, Azam ilijibu mapigo kwa kusawazisha kupitia kwa Mudathir aliyeingia kipindi cha pili, kiungo huyo alipokea pasi ya Tchetche na kupiga shuti akiwa ndani ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Simba.
Azam iliyovuliwa ubingwa wa ligi na mabingwa wapya Yanga Jumatatu iliyopita, ilifanya mabadiliko dakika ya 67 kwa kutoka Kavumbagu na kuingia nahodha John Bocco aliyetoka kwenye majeruhi.
Simba ilimaliza mchezo huo dakika ya 74 kwa kupata bao la pili lililofungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ baada ya kupiga krosi iliyodunda chini na kutinga wavuni moja kwa moja, Messi alifunga akitumia vema pande la Mkude.
Mwamuzi alilazimika kumwonyesha kadi ya njano Messi baada ya kushangilia bao hilo kwa kuvua jezi yake. Licha ya dakika saba kuongezwa kufuatia dakika 90 kumalizika, Simba ilimaliza mpira huo kwa ushindi huo.
Oscar Assenga kutoka Uwanja wa Mkwakwani, Tanga naye anaripoti kuwa, wenyeji Coastal Union wamefanikiwa kujiondoa kwenye janga la kushuka daraja baada ya kuichapa Stand United mabao 3-1 na kufikisha pointi 31.
Mabao ya Coastal yaliyoiweka kwenye hali mbaya Stand yamefungwa na Ayoub Semtawa dakika ya 17, Yusuph Chuma (dk 42) na Mnigeria, Bright Obina (dk 69), huku lile la Stand likifungwa na Mnigeria, Chidiebere Abisirim.
Kutoka kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro wenyeji Mtibwa Sugar wameilaza Ruvu Shooting mabao 2-0 na kuiweka pabaya zaidi timu hiyo ya jeshi kwenye janga la kushuka daraja ikiwa na pointi 29.