27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda: Tuwalinde vijana na dawa za kulevya

Mizengo-PindaNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewaomba viongozi wa dini nchini waitumie mikutano yao ya mahubiri kutoa elimu juu ya athari za dawa za kulevya kwa waumini wao na Watanzania wote kwa ujumla.
Wito huo ameutoa jana Dar es Salaaam, alipokuwa akizungumza na viongozi na waumini wa Kanisa la Moravian Tanzania kwenye ibada ya uzinduzi wa Jimbo la Mashariki la kanisa hilo uliofanyika makao makuu ya jimbo hilo, Mbagala Chamazi.
“Niwaombe sasa viongozi wa dini tuungane na Serikali kutoa elimu juu ya athari za biashara ya dawa za kulevya na matumizi yake katika jamii.
“Ninawasihi viongozi wa dini tuanzie makanisani na misikitini, na kwenye mikutano yote tunayoifanya; tusimalize mikutano yetu bila kutoa elimu kuhusu athari za dawa za kulevya kwa waumini wetu na umma kwa ujumla.
“Viongozi wa dini mna jukumu kubwa la kuwalea zaidi vijana ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wao ndiyo kundi kubwa zaidi miongoni mwa waumini wenu. Ninaamini tukishirikiana kutoa elimu hii pamoja, tutaweza kuwaokoa vijana wetu ambao ndiyo waathirika zaidi,” alisema.
Alisema jimbo hilo jipya linalojumuisha mikoa mitano ya Dar es Salaam, Morogoro, Lindi, Mtwara na Pwani lina jumla ya wakazi 9,817,207 kwa mujibu wa Sensa ya Makazi na Watu ya mwaka 2012. Pia lina ukubwa wa kilometa za mraba 190,646 sawa na asilimia 20.1 ya eneo lote la Tanzania.
“Kati ya wakazi hao, asilimia 56.8 ni watu wenye umri wa kufanya kazi yaani kuanzia miaka 15-64, wengi wao wakiwa ni vijana. Pia kuna asilimia 38.1 ambao ni watoto wenye umri chini ya miaka 15 na waliobakia ni wazee wenye miaka 65 na zaidi sawa na asilimia 5.1,” alisema.
Aliutaka uongozi wa kanisa utumie fursa zilizopo kwenye mikoa hiyo za kilimo, madini na gesi asilia kwa kuwahamisha waumini wake na kuwabadilisha kifikra ili wazitumie fursa hizo kujiletea maendeleo na kujikomboa kiuchumi.
Akizungumzia kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Pinda alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini washirikiane na Serikali kukemea kwa nguvu zote vitendo hivyo vya kikatili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles