Na CHRISTINA GALUHANGA-
DAR ES SALAAM
TAASISI ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC) imewataka wanahabari nchini kutumia taaluma zao kuelimisha jamii umuhimu wa kunyonyesha mtoto maziwa halisi ya mama.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa TFNC, Dk. Joyceline Kaganda, alisema jamii hasa maeneo ya vijijini haina uelewa na umuhimu wa kunyonyesha.
Alisema wanawake waliopo kwenye mfumo rasmi wa ajira, wanapata nafasi ya kunyonyesha kiwango kinachotakiwa tofauti na wa sekta binafsi.
Alisema ni muda mwafaka sasa wanaume kuwapa kipaumbele wake zao.
“Wanawake wengi wamejikuta wanashindwa kunyonyesha kiwango kinachotakiwa kwa sababu ya kazi ngumu wanazofanya bila kula chakula kinachohitajika ambacho kitamsaidia mtoto kumpa maziwa ya kutosha,” alisema Dk. Joyceline.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa kunyonyesha, ndiyo maana Serikali iliamua kutunga sheria inayomlinda mwanamke na mtoto kwa kumpa mapumziko ya siku 84 baada ya kujifungua na mwenye mapacha siku 100.
Alisema sheria hiyo imesaidia kumpunguzia mwanamke kazi ngumu hasa miezi sita ya mwanzo.
Ofisa Habari wa Elimu kwa Umma wa TFNC, Herbert Gowele alisema takwimu za unyonyeshaji zimepanda kutoka asilimia 41 mwaka 2012 hadi 59 sasa.
Alisema utafiti wa afya ya mama na mtoto na viashiria vya malaria kwa mwaka 2015/16, unaonyesha wanawake wananyonyesha watoto wao tofauti na siku za hivi karibuni.
“Kuna imani potofu za baadhi ya wasichana wanaokataa kunyonyesha, huku wengine wakiwa wanatumia simu za kiganjani wakati wa kunonyesha jambo ambalo linasababisha watoto kushindwa kunyonyesha kiwango kinachotakiwa,”alisema Gowele.