29.3 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

TAHARIRI: WAJUMBE CHAGUENI VIONGOZI SAHIHI TFF

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), umepangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma na wagombea wa nafasi mbalimbali wanasubiri muda wa kampeni uanze ili waanze kunadi sera zao.

Uchaguzi huu unafanyika baada ya uongozi uliopo madarakani chini ya Rais Jamal Malinzi kufikia ukomo wake, hivyo kuruhusu kufanyika ucahaguzi mwingine kwa mujibu wa katiba ya TFF.

Uchaguzi huu ni ishara kuwa Tanzania itapata viongozi wengine watakaochaguliwa kuliongoza soka la Tanzania kwa kipindi kingine cha miaka minne ijayo.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF ambao ni wapiga kura katika mkutano huo, wao ndio wana jukumu la kuchagua viongozi sahihi kwa ajili ya mustakabali wa soka la Tanzania.

Sisi MTANZANIA tunauangalia uchaguzi huu kwa undani zaidi kwa kuwa ndio unaochagua viongozi watakaowakilisha katika vikao vya maamuzi vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Hivyo ni jambo linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee kwa kuwaasa wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF, kutumia uzalendo na umakini wao katika kuchagua viongozi watakaolifikisha soka la Tanzania katika mafanikio bora zaidi.

Ni wakati wa wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF wawe na umoja na uzalendo kwa Taifa lao kwa kuchagua viongozi wenye weledi na wenye uchungu na maendeleo ya soka la Tanzania.

Sisi MTANZANIA tunawatakia wajumbe wote wa mkutano mkuu wa TFF, kuwa na uzalendo na nchi yao kwa kuchagua viongozi watakaoendeleza soka la Tanzania kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Watanzania wanapenda soka na wanatamani mafanikio ya kuona timu yao ya Taifa ikifanya vizuri katika Fainali za Afrika na hata Kombe la Dunia.

Kama wajumbe wataweka masilahi yao binafsi kwa viongozi watakaowachagua, wakaweka nyuma uzalendo wa Taifa lao kwa kuchagua viongozi wasio na sifa, yatakuwa majuto kwao na Watanzania wote.

Tukumbuke kuwa viongozi watakaochaguliwa Agosti 12 mjini Dodoma, watakuwa na majukumu mazito ya kusimamia soka la Tanzania, hivyo ni jambo linalohitaji wajumbe kutumia hekima na busara zao katika kuchagua viongozi watakaotutoa katika sehemu moja na kutufikisha kwingine.

Bila shaka wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF ni watu waelewa na wanafahamu Taifa linahitaji viongozi wa namna gani ambao watafanya kazi kwa kasi ya kuleta maendeleo bora zaidi.

Tuwatakie utulivu, amani na uzalendo wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF ili waweze kutimiza vema jukumu lao la kuchagua viongozi walio wazalendo na uchungu na soka la Tanzania kwa kipindi cha miaka minne ijayo watakachokuwa madarakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles