27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

GADIEL MICHAEL, SINGANO ‘WAPIGWA CHINI’ SAFARI YA UGANDA

Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Azam FC umeweka wazi kuwa, wachezaji wake watatu, Gadiel Michael, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Shaban Chilunda, hawatakuwamo katika safari ya kikosi hicho kitakachopaa leo kwenda nchini Uganda.

Wachezaji hao wataachwa kutokana na sababu mbalimbali zinazowakabili. Gadiel anatajwa kuwa mbioni kujiunga na Yanga, Singano bado hajaungana na wenzake tangu alipotoka   Morocco baada ya kushindwa kukamilisha usajili wa kuichezea Difaa Al Jadid, huku Chilunda akikosa safari hiyo baada ya kuwa majeruhi.

Azam inatarajia kuondoka na kikosi cha wachezaji 26, kuelekea Uganda kwa ajili ya kambi hiyo ambayo watacheza michezo minne ya kirafiki dhidi ya timu za URA, SC Villa, Vippers na mabingwa wa soka nchini humo, timu ya KCCA, inayomilikiwa na Manispaa ya Jiji la Kampala.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Meneja wa kikosi hicho, Philip Alando, alisema timu hiyo inatarajia kuondoka leo kuelekea Uganda ambako wataweka kambi ya siku 10, kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu.

“Tunatarajia kuondoka usiku wa kuamkia kesho (leo) tukiwa na kikosi cha wachezaji 26, wachezaji saba hatakuwa sehemu ya safari hiyo kutokana na sababu mbalimbali, wachezaji hao ni pamoja na Gadiel, Singano na Chilunda.

“Kambi yetu itamalizika rasmi Agosti 15, mwaka huu, baada ya hapo tutaanza safari ya kurejea nchini tayari kwa mchezo wetu wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Ndanda FC, utakaochezwa katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara,” alisema Meneja huyo.

Timu hiyo tayari imecheza michezo mitano ya kirafiki hadi sasa, michezo hiyo ni dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, Njombe Mji FC, Lipuli FC, Mbeya City na KMC, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Katika michezo hiyo, Azam imeshinda michezo miwili dhidi Lipuli FC na KMC, kufungwa miwili dhidi ya Njombe Mji na Rayon Sports, huku wakitoka sare na Mbeya City.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles