Na MWANDISHI WETU
ASILIMIA kubwa ya jamii za Kiafrika hulea familia kubwa kuzidi uwezo wao kifedha. Hapa namaanisha kuwa na familia zaidi ya mama, baba na watoto. Wazungu wanasema extended families. Maisha ya namna hii husababishwa na hali ya umaskini wa kipato kwa baadhi ya familia zetu.
Watu wengi waliopitia maisha haya walidhani ipo siku yataisha, lakini jambo hili ni gumu kuisha ikiwa vipato vya wanafamilia havijaimarika. Ili kumaliza tatizo hili ukiwa baba au mama mwenye nyumba basi wewe ndiye mwenye uamuzi wa kumaliza au kubadilisha hali hiyo hapo kwako.
Nimeshuhudia baadhi ya familia zikipata taabu kwa ajili ya kuwahudumia ndugu wa aina hii, inapofikia hatua mgeni wa hapo nyumbani kwako unamkabidhi chumba cha watoto wako na wewe unaishia kujibana na watoto kwenye chumba kimoja ukihofia kuwalaza na mgeni, hii ni hali mbaya mno.
Kwa jinsi maisha yalivyo sasa, watu wengi wamekuwa na tabia ambazo hazitabiriki, kiasi kwamba mzazi unaogopa kumlaza mtoto wako na mgeni yeyote atayekuja hapo ndani ukihofia jambo lolote baya analoweza kumfanyia mwanao. Hali kama hizi zimesababisha watu wengi kuviacha vyumba vya watoto wao na kuwaachia wageni ambao wamekuja hapo nyumbani kutumia vyumba ambavyo viliandaliwa mahususi kwa ajili ya watoto lakini vinatumiwa na wageni, huku watoto wakiendelea kuchangia vyumba na wazazi wao na wasijue ni lini wataweza kuvipata vyumba vyao.
Kwa kweli hali kama hii inarudisha nyuma maendeleo kwani ni ndoto ya kila mzazi kuishi kisasa zaidi, nikiwa na maana kwamba kila mtoto kuwa na chumba chake. Lakini kwa walio wengi bado ni ndoto, wanakwamishwa na ndugu na jamaa ambao wengi wao bado ni tegemezi kwa familia zao.
Hivyo basi, kama wewe ni mmoja wa wageni unayeishi katika familia za aina hii hebu chukua hatua ya kutafuta ni namna gani utaweza kujitegemea na kuwapa fursa watoto na wanafamilia angalau baada ya miaka kadhaa ya kusota chumbani kwa baba na mama hatimaye warudie vyumba vyao.
Sikatazi watu kutembelea ndugu zao, lakini ifike mahali unapofikia umri wa kujitegemea jaribu kutafuta kazi na kuanza maisha yako ili kuwapunguzia wenzio mzigo.