NA SHERMARX NGAHEMERA,
UJAJI wa Kiwanda cha Dangote katika soko la saruji nchini umeonekana kuvuruga mwenendo wa soko, kwani bei yake ni ya chini kwa asilimia 40 ukilinganisha na ile inayotengenezwa nchini kwa miaka yote, vingine vina umri wa miaka 50.
Dangote Cement kilichoko Mtwara ni ‘mwali mpya mtaani’ na ujaji wake umeleta shida pamoja naye kulalamika hapo awali kuwa Serikali haijatekeleza baadhi ya ahadi zake.
Wachunguzi wa mambo wanadai kuwa, utitiri wa viwanda ambavyo vimefika idadi yake kuwa nane unahitaji kuratibiwa, vinginevyo ni vurugu, kwani soko ni moja na hivyo kudai viwango vinavyolingana na kuweka nidhamu katika soko.
Hata hivyo, viwanda kongwe viwili vya saruji nchini, kile cha Twiga na Simba vimeapa kupambana kulinda maslahi yao na kutumia ukongwe wao kushinda katika medani ya vita sokoni. Wanasema Dangote ametukuta na hivyo sio shani kumkimbia, kwani soko ni huria na lina nafasi kwa kila mtu na isitoshe wao ni waumini wa ushindani.
Lakini hiyo ni rahisi kusema na sio kutenda, kwani saruji hiyo imeanza kutishia sokoni viwanda vya siku nyingi nchini, kikiwamo cha Tembo (Lafarge’ Mbeya Cement) kwa kuongeza ushindani na kupunguza kiwango cha faida kwa wazalishaji wenye mtandao mpana katika eneo la Afrika Mashariki yote.
Aliko Dangote, ambaye ni tajiri namba moja Afrika, ana sera zinazopingana na viwanda vingi katika eneo hili kwa kutaka mauzo kwa wingi kwa bei nafuu ya kuwezesha watu kujenga nyumba zao badala ya kuuza chache kwa bei kubwa na kufanya saruji kuwa ni ya miradi pekee.
Vunja bei inasemekana kumfanya yeye kushinda washindani wake na kufikia hapa alipo kama tajiri namba moja Afrika. Kule kwao Nigeria analaumiwa kwa kuvunja bei kila biashara anayoingia. Inasemekana hapendwi kabisa na wafanyabiashara wa huko.
Amekuwa akiwaangusha wenziwe wenye mitazamo ya kizamani ya kinyonyaji na kuwashinda vibaya, kwani anatumia viwanda vyake kwa kufanya kuwa vyenye mrengo wa kieneo (regional) badala ya kinchi moja moja. Ametanuka katika mawanda mapana.
Kwa Kenya bei ya saruji ya Dangote iko bei ya chini kwa kiasi cha asilimia 20 hadi 40 na hivyo kuwa vunja bei na kufanya bei kuanguka kwa kipindi zaidi ya mwongo mmoja. Dangote ana viwanda Tanzania, Kenya na Ethiopia Ana mipango ya kujenga kiwanda cha saruji mjini Jinja, nchini Uganda.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Cement nchini Ethiopia, Onne Van der Weijde, anasema wanaangalia kwa makini kile kinachotokea katika eneo hili na kuhakikisha kuwa bado wana lengo na nia ya kuwa wachezaji wakuu wa bidhaa hiyo katika Afrika na ulimwengu.
Anasema wamefarijika na mwenendo wa serikali ya Ethiopia kwa kuwa na miradi mingi ya ujenzi, ikiwamo reli na uboreshaji miundombinu, mtandao wa umeme, makazi na usafirishaji wa mijini ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mahitaji ya saruji na hivyo mauzo ya kampuni yao na kufikia kiasi cha asilimia 28 ya soko toka wafungue kiwanda cha Mugher chenye uwezo wa tani milioni 2.5 mwaka jana.
Mauzo yamepanda katika Afrika Mashariki na Kusini kutoka dola za Marekani milioni 54.5 mwaka jana hadi milioni 82.2 mwaka huu miezi sita ya mwanzoni.
Mahitaji kama hayo ya saruji yako Tanzania kwa maana ya Reli ya Kati (SGR), barabara za juu na za mwendokasi na ujenzi wa bwawa la umeme Stiegler, Mtambo wa LNG Lindi na Kiwanda cha Mbolea Kilwa na hivyo kuwa na matarajio ya biashara nzuri nchini inayohitaji saruji.
Vunja bei
Mauzo yake mazuri na kuweza kupata faida ya dola za Marekani zaidi ya milioni 4 imefanya kampuni ya Dangote kutoa bei poa kwa saruji yake nchini Kenya na Ethiopia na hivyo kutishia masoko hayo kwa urahisi wake.
“Bei ya saruji ya Dangote katika Ethiopia kwa mfuko wa kilo 50 ni dola 8.60, wakati Dangote anauza dola 6.90,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Lakini Ofisa Mtendaji Mkuu, Sada Ladan-Baki, anatetea hali hiyo kwa kusema vunja bei inatokana na ahadi yao kwa jamii ya Afrika ya kushiriki kusaidia kuboresha miundombinu na kuongeza uwezo wa kupunguza tatizo la ujenzi wa makazi barani humu.
Hali hiyo wezeshi nayo inaungwa na uwepo wa kuongezeka uwezo wa uzalishaji kutoka tani 922,000 mwaka jana hadi tani milioni 1.6 kwa miezi sita ya mwanzo mwaka huu.
Bei ya wastani ya rejareja nchini Kenya kwa mfuko wa saruji kilo 50 ni dola 4.70 kutoka dola 7.40 kabla ya ujio wa Dangote mwaka jana.
Hapa nchini Dangote anauza saruji yake kwa bei ya dola 4.50 (Sh 9,900) ambayo ni anguko la bei la maridhawa kutoka bei ya awali ya dola 5.85 (Sh 12,870), ambayo ni nafuu kwa asilimia 20 na uzuri wake ni kuwa saruji inauzwa hivyo mlangoni kwake mteja na sio kuifuata kiwandani. Ni nafuu iliyoje!
Nchini Uganda, bei ya saruji mwishoni mwaka jana ilikuwa dola 8.80, ambapo Dangote hajaanza shughuli, kwani amepania kujenga kiwanda nako. Safari ya Museveni kutembelea viwanda nchini haikuwa ya bure, bali na malengo mahsusi.
Mahusiano mazuri, upole, uungwana na pale anapofanyia kazi ni kivutio kikubwa kwa wengi na hufanya mambo yake yanyooke na hata katika mazingira magumu. Serikali ya Ethiopia kuvutia uwekezaji wake, hapo ilimpa umeme wa uhakika katika bei poa iliyolegezwa (discounted) ya dola 0.03 kwa kWh. Kwa kufanyiwa hivyo, Dangote bei zake zilipungua kwa asilimia 40, ukifananisha na bei ya kule Nigeria.
Dangote katika kiwanda chake cha Mtwara anatengeneza saruji ya daraja la 32.5, wakati akisubiri kuidhinishiwa kwa ubora wa saruji daraja 42.5 na mamlaka za Tanzania. Kampuni inategemea kuwa na soko la asilimia 23 kufikia mwezi huu na bei ni dola 80 kwa tani nchi nzima, ingawa kuna uhaba wa dizeli na gharama kubwa za usafiri kutokea Mtwara.
Dangote ina mipango ya kujenga viwanda viwili Rwanda na vitatu jijini Dar es Salaam na kimoja Burundi na Jinja Uganda. Kuhusu Kenya atajenga kiwanda pale Kitui, ambacho kitakuwa na uwezo wa tani milioni 3 na kutegemewa kufunguliwa 2019.
Soko la saruji shindani
Miamba wawili, Dangote na Lafarge’ wanapambana kwelikweli kushikilia soko la Afrika la saruji na ushindani huu kuleta tija na ajira kwa bara hili ambao uchumi wake umeanza kukua kwa kasi.
Soko la saruji Afrika Mashariki linatawaliwa na Lafarg’e Holcim kwa kuwa na asilimia 27 ya soko, wakati Tororo Cement ina asilimia 21 na ARM (Athi River Cement) asilimia 17. Katika Afrika Lafarge’ Holcim ni mzalishaji mkubwa, akiwa na uwezo wa tani milioni 50 kwa mwaka, akifuatiwa karibu na Dangote Cement akiwa na tani milioni 47.
Viwanda sita kujengwa
Ukiachia ahadi ya viwanda vitatu kujengwa na Dangote, Tanzania imepata maombi na kukubali viwanda vingine vitatu kutoka kwa wawekezaji wengine watatu, wakiwamo kampuni za EAM, Mamba na Sungura.
Uwekezaji huo utaifanya Tanzania iwe na uwezo wa uzalishaji kwa ujumla wake nchini kuwa tani milioni 17.
Kutokana na maelezo ya Waziri wa Biashara na Viwanda, Charles Mwijage, kampuni hizo ziko tayari kuwekeza Sh trilioni 20 kuzalisha saruji miaka michache ijayo, ila waruhusiwe kuuza saruji yao nje ya nchi, naye amekubali sharti hilo.
Alifafanua kuwa, EAM Company alitaka kujenga kiwanda chake huko Tanga na kuzalisha tani hadi milioni 7 kwa mwaka.
Wazalishaji katika sekta ya saruji ni Twiga, Simba, Tembo, Nyati na Camel, ambayo jumla uzalishaji wao ni tani milioni 10.3 na wakijumlisha na ule wa EAM wa milioni 7 itafanya uzalishaji kufikia tani milioni 17 na ukijumlisha na Dangote wa tani milioni 3 inafanya iwe milioni 20.
Mwijage alibainisha kuwa, nchi hadi sasa ina uwezo uliofungwa (installed capacity) wa tani milioni 10.3, lakini inayotumika ni tani milioni 7 tu, ikiwa ni asilimia 68 ya uwezo.
Kiwanda kingine kikubwa cha kuzalisha saruji kinatarajiwa kujengwa mkoani Tanga cha kampuni ya Hengya Cement kutoka China, chenye uwezo wa tani milioni 3 kwa mwaka kama kile cha Dangote Mtwara na hivyo kuwa mojawapo wa kiwanda kikubwa Afrika.
Hengya Cement Company kitakuwa kiwanda kitakachokuwa na uzalishaji mkubwa barani Afrika na kitaleta ushindani mkubwa katika soko la saruji nchini na kinatarajiwa kuwekeza dola bilioni 2.5 nchini kwa maelezo ya awali ya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Clifford Tandari na kinatarajiwa kutoa ajira 10,000 za moja kwa moja, takwimu ambazo zilirudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella.
Kiwanda cha saruji kitaleta ushindani mkubwa kwa kiwanda cha Dangote Cement kilichopo Mtwara ambacho ni kiwanda kikubwa Afrika Mashariki, kitakachozalisha tani milioni 3 katika ukamilifu wake.
Wawekezaji wanavutika na hali na masharti mazuri ya uwekezaji nchini kwa kupata mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
Matatizo Saruji Tanga
Kiwanda cha kuzalisha saruji cha Tanga (Simba Cement), mojawapo ya viwanda vikongwe nchini cha kuzalisha saruji kimeainisha matatizo lukuki ya utendaji.
Kiwanda hicho ni kinara wa uchumi mkoani Tanga kupitia kodi pamoja na kutoa fursa ya ajira kwa wananchi.
Isitoshe, hutengeneza saruji bora katika nchi za Afrika Mashariki kwa kukidhi viwango vya ubora duniani, kwa maelezo ya Mkurugenzi wake, Reinhardt Swart.
Hata hivyo, anatatizwa na mwelekeo wa shughuli za uzalishaji, licha ya dhamira nzuri ya serikali ya awamu ya tano ya kuja na sera ya uchumi wa viwanda. Anasema kama changamoto za kisera na kimiundombinu hazitaweza kufanyiwa kazi, sera hiyo inaweza kushindwa kutekelezeka.
Kwani anasema kuwa serikali imejikita zaidi katika uanzishwaji wa viwanda vipya badala ya kuboresha mazingira bora ya viwanda vilivyopo viweze kuimarika.
“Sera ya uchumi wa viwanda ni nzuri, lakini naona serikali imejikita katika uanzishwaji wa viwanda vipya, hivyo naona kutakuwa na anguko kubwa la viwanda vya zamani,” anabashiri Mkurugenzi Swart.
Hivyo anaishauri serikali kuwa ni vema kwanza ingetatua changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda vya saruji kwa sasa ili vilivyoko viendelee kuwepo kwa muda mrefu, badala ya kunyong’onyea na mwishowe kufa.
Ili Tanzania ifanikiwe katika azma yake ya uchumi wa viwanda, ni lazima ihakikishe inatoa kipaumbele kwa wawekezaji wazawa kuwekeza zaidi katika sekta binafsi.
Mkurungenzi huyo bila kumung’unya maneno, aliweka bayana baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo, kuwa ni uhaba wa nishati ya umeme usiyoaminika na kutotosheleza na kuwalazimu kutumia nishati mbadala iliyo ghali ili kuendelea na uzalishaji.
“Tunatumia umeme katika mitambo yote, lakini uliopo ni mdogo na hivyo kusitisha uzalishaji ili kufidia gharama ya ziada za uzalishaji umeme kiwandani hapo,” amebainisha Swart.
Kuna changamoto ya miundombinu ambayo gharama za usafirishaji humuathiri mnunuzi wa mwisho wa bidhaa hiyo na kufafanua kwamba;
“Licha ya kwamba saruji inayozalishwa nchini ilipaswa iuzwe kwa bei sawa na bure, lakini gharama za usafirishaji ni kubwa kutokana kuwepo kwa miundombinu ambayo siyo rafiki,” amebainisha Swart.
“Tulipanga kutumia njia ya reli kwa ajili ya kusafirisha shehena ya mizigo, lakini bado huduma hiyo haipo katika maeneo mengi nchini, hivyo shehena nyingine hulazimika kutumia barabara ambayo ni ghali sana; na kama huduma ya reli itaboreshwa na kuwa ya uhakika, tunaweza kuachana na kutumia usafiri wa barabara, kwani ni ghali sana.”
Changamoto nyingine ni kuwepo kwa saruji kutoka nje ya nchi, hali inayosababisha wazalishaji wa ndani kukosa soko la bidhaa zao kutokana na ukweli kuwa, saruji inayotoka nje huuzwa kwa bei nafuu, tofauti na inayozalishwa nchini, kwani hawalipi kodi kwao.
“Licha ya serikali kuongeza kodi kwa saruji kutoka nje, bado tatizo ni kubwa, kwani viwanda vya humu nchini vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 4.8, huku soko likihitaji tani milioni 3 pekee, hivyo kuna kiasi kikubwa cha saruji kinabaki bila ya soko,” amebainisha Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Lakini mahitaji ya saruji yanaongezeka kufuatia shughuli za uchumi kuongezeka na wachunguzi wanadadisi hofu ya Swart.