WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Ofisa katika Ofisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Kiyabo kuwakamata wajumbe wa bodi, waliokuwa wakurugenzi na viongozi wa Halmashauri ya jiji la Mbeya 12 kwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 63 katika ujenzi wa soko jipya la Mwanjelwa.
Waziri Majaliwa ametoa agizo hilo leo Jumatatu Julai, 30 wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri za Wilaya ya Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini.
Amesema ripoti ya ukaguzi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2015/16 imeonyesha halmashauri hiyo kupitia viongozi wake walishiriki kuomba mkopo wa Sh bilioni 13 ili kujenga soko la Mwanjelwa katika benki ya CRDB bila idhini ya ofisi ya hazina na kusababisha riba deni hilo kufikia Sh bilioni 63.
Majaliwa amewataja viongozi hao kuwa ni wajumbe wa Bodi Mussa Mapunda, Devis Mbembela, Lydia Abasi na Samwel Bubegwa.
Aidha, mbali na wajumbe wamo pia waliowahi kuwa wakurugenzi wa jiji hilo Mussa Zungiza (mkurugenzi wa jiji msaatafu), Athanase Kapunga (meya mstaafu wa jiji la Mbeya), Elizabeth Munuo (mkurugenzi wa jiji mstaafu) Dk. Samwel Lazaro (aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi) ambaye kwa sasa ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
“Hawa watu kama wapo hapa Kamanda wa Takukuru majina yao haya hapa hatuwezi kuwa na watumishi ambao wanaweza kufanya uamuzi wa kuitia hasara serikali, kama hawapo hapa watafutwe wakamatwe wahojiwe na wafunguliwe mashtaka, ili wajue mtu akiamua kuchezea fedha za umma atakamatwa,” amesema Majaliwa.