30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AAGIZA VIGOGO 12 MBEYA WACHUNGUZWE

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

Na AZIZA MASOUD-MBEYA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  Mkoa wa Mbeya,  Emanuel Kiabo, kumkamata na kumhoji Atanas Kapunga, aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya na wenzake 11 kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 63.448.

Alitoa agizo hilo jana mjini hapa  alipozungumza na watumishi wa Halmashauri za Wilaya ya Mbeya na   Jiji la Mbeya.

“Serikali hii haiwezi ikawaacha watu hawa ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa halmashauri moja.

“Kama wako humu ndani naagiza wakamatwe na waanze kuhojiwa na ambao wamestaafu au kuhamishwa vituo vya kazi wasakwe popote walipo ili nao waje kuhojiwa,” alisema.

Mbali na Kapunga, wengine wanaotakiwa kukamatwa na kuhojiwa ni waliowahi kuwa wakurugenzi wa Jiji la Mbeya kwa nyakati tofauti, Mussa Zungiza, Elizabeth Munuo, Juma Idd na Dk. Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukurugenzi.

Wengine ni aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji hilo, James Jorojik   na waliokuwa wajumbe wa bodi ya zabuni ambao ni Mussa Mapunda, Samweli Bubengwa, Davis Mbembela, Lydia Herbert na Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya mradi huo bila kuzingatia maslahi ya jiji.

Mwingine ni Emily Maganga ambaye inasemekana hakuishauri vizuri bodi hiyo.

Katika maelezo yake, Waziri Mkuu alisema watumishi hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahiki za  sheria kwa kuwa wameisababishia Serikali hasara kupitia mradi wa ujenzi wa Soko la Mwanjelwa ambalo hadi sasa halijaonyesha faida.

“Mradi huo wa soko ulighubikwa na changamoto nyingi kuanzia hatua za awali kwani hata uchukuaji wa mkopo haukuwa umezingatia mpango mkakati wa biashara kwa sababu  ulisababisha halmashauri ya jiji kuchukua mkopo zaidi ya kiasi kilichokusudiwa.

“Mbali na kuzidisha kiasi cha mkopo, pia baada ya kukamilika   ujenzi watuhumiwa hao walighushi mikataba ya upangaji, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya sheria ya ununuzi ya umma.

“Pia watuhumiwa hao waligawa vizimba kwa wafanyabiashara bila kupitia mchakato wa ununuzi, jambo ambalo haliwezi kukubalika.

“Yaani hata waathirika walikuwa sokoni hapo, awali kabla ya kuungua kwa soko hilo, hawakupewa kipaumbele katika mchakato wa upangishaji wa soko jipya wakati kwa hali ya kawaida  ilitarajiwa wangekuwa wa kwanza kufikiriwa kutokana na hasara waliyoipata baada ya kuunguliwa mali zao,” alisema Waziri Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles