Na Tobias Nsungwe – Dar es Salaam
WIZARA ya Fedha na Mipango imetiliana saini na kampuni ya ujenzi wa barabara ya Reynolds kw ajili ya ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara mkoani Morogoro.
Barabara ya kilometa 67 itajengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh bilioni 101 kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), Marekani na Uingereza.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango, ilisema mkataba huo ulisainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shaaban na Benjamin Arbit ambaye ni mkandarasi kutoka Kampuni ya Reynolds.
Taarifa hiyo imesema ujenzi wa barabara hiyo utahusisha ujenzi wa daraja katika Mto Ruaha na itasaidia wakulima wadogo kupitia Mpango wa Uendelezaji Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kaika Bonde la Mto Kilombero ambao wataweza kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao.
“Kuimarika kwa kipande hiki cha barabara kutaongeza uzalishaji wa nafaka na bidhaa nyingine hatimaye kupunguza gharama za chakula na umasikini wa wananchi.
“Ujenzi wa miundombinu unalenga kuchochea maendeleo ya kilimo cha biashara kwa kuwa utasaidia kuwakutanisha wafanyabiashara na wakulima,” alisema Amina.
Alisema barabara ya Kidatu hadi Ifakara ndiyo inayounganisha wilaya za Kilombero na Ulanga na ni barabara kuu inayokwenda Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Balozi wa EU hapa nchini, Roeland van de Geer, aliahidi kuwa EU UKAID na USAID, zitaendelea kushirikiana kwa kiwango cha juu na Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya ujenzi na miundombinu kwa ujumla.
Alisema atahakikisha EU inachangia katika kupata soko la uhakika la mazao ya kilimo.