25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

MABAKI MIFUPA YA BINADAMU MWANZA YAMKERA WAZIRI

Na BENJAMIN MASESE-MWANZA


SERIKALI imesikitishwa na kitendo cha  mifupa ya binadamu kuzagaa katika makaburi ya Kitangiri na Igoma mkoani Mwanza.

Imesema ni aibu  kwa uongozi wa Jiji la Mwanza kushindwa  kuchukua hatua kutenga maeneo mengine ya maziko.

Pia imegundulika asilimia 95 ya  migogoro ya ardhi iliyopo mkoani hapa inahusu  madai ya fidia ya Sh bilioni 8.

Hayo yamegundulika jana,wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, alipokuwa akizungumza na watumishi wa jiji Idara ya Ardhi kutembelea maeneo mbalimbali ya wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Akiwa Nyamagana, Waziri Mabula alipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi, Hosiana Kusiga, kuwa asilimia 95 ya migogoro ya ardhi inahusu fidia, huku uwezo wa  jiji hilo kulipa ni mdogo, hali iliyosababisha maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kijamii kuendelezwa.

“Mheshimiwa kuna tatizo kubwa kwetu, makaburi yote yaliyokuwa yametengwa kipindi cha nyuma yamejaa,uwezo wa Jiji kulipa fidia maeneo yaliyotengwa hatuna kabisa… ndiyo maana asilimia 95 ya migogoro  inahusu fidia, zinahitajika zaidi ya Sh bilioni nane ili kumaliza tatizo hili,”alisema Kusiga.

Kutokana na taarifa hiyo,Naibu waziri alisema, “tena umenikumbusha kitu, natoka Ilemela nimekuwa nikipita pale makaburi ya Kitangira mpaka nashikwa na hasira, mifupa imetapaa, watu wanazikwa juu ya wengine, hivyo hivyo makaburi ya Igoma, hii ni aibu kubwa ndani ya Jiji la Mwanza.

“Haiwezekani mkashindwa kuwasitiri wenzetu walioitwa na Mungu, hakikisheni mnapopima aradhi wekeni maeneo ya makaburi na mlipe fidia, tunakoelekea ni kuleta ugomvi makaburini maana itafikia ndugu watazuia kaburi la mtu wao lisifukuliwe, chukueni hatua haraka,”alisema.

Kutokana na hali hiyo, alitoa miezi mitatu kwa watumishi kuhakikisha wanarasimisha makazi yote na kutoa hati miliki kabla ya Serikali kutangaza mpango mji.

Aliuagiza uongozi wa Jiji kutafuta eneo jingine na kulipatia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)  ili kujenga  nyumba za watumishi wa Serikali.

Kwa upande wa Meneja wa NHC   Mkoa wa Mwanza, Benedict Kilimba alisema amekuwa akiumiza kichwa  juu ya kupata eneo la kujenga mji wa makazi bora ya kisasa ‘setlite City’ ambapo aliutaka uongozi wa jiji hilo kuendelea  kuwatafutia maeneo yasiyo na mgogoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles