MAJALIWA ATAKA MGOGORO WA ARDHI UMALIZWE

0
631

Na Mwandishi Wetu, Mbeya


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa maelekezo ya namna ya kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka sita, kati ya uongozi wa Kiwanda cha Saruji Mbeya na wananchi wa kijiji cha Nanyala, wilayani Mbozi.

Mgogoro huo, umetokana na Kiwanda cha Saruji Mbeya kupewa  eneo la kijiji hicho chenye ekari 2,315 na uongozi wa Mkoa wa Mbeya bila ya makubaliano na wanakijiji hali iliyosababisha wagome kuondoka.

Pia Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa mikoa ya Songwe, Luteni mstaafu Chiku Gallawa  na Amos Makalla  wa Mbeya kukutana na kufanya mazungumzo ya kulirudisha eneo hilo.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana,baada ya wananchi wa kijiji hicho kuzuia msafara wake kwa lengo la kumwelezea changamoto ya kudhulumiwa ardhi yao na kukabidhiwa kwa mwekezaji bila ya kushirikishwa.

Alisema Serikali  ni sikivu na inawajali wanyonge, ndiyo maana amesimama ili aweze kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi, hivyo amewaomba  waendelee kuiamini na watarudishiwa ardhi yao.

Aliagiza Kampuni ya Saruji Mbeya kuondoa kesi iliyoifungua mahakamani dhidi ya wananchi wa eneo hilo ili waweze kukutana na Serikali pamoja na wananchi hao kwa ajili ya kujadili namna bora ya uwekezaji katika eneo hill.

Alisema kiwanda hicho kilipewa eneo hilo la Mkoa wa Songwe kimakosa na Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kupata malighafi ya kutengenezea saruji.

“Hatuzuii kiwanda kufanya kazi ila tunataka mkubaliane na wananchi kwanza ili kuondoa migogoro. Wananchi wanahitaji viwanda ila si kwa migogoro. Wananchi nawaomba muendelee kuwa na amani na hakuna atakayechukua ardhi yao bila ya ridhaa yao.”

Kwa upande wake, Gallawa alishukuru uamuzi wa Waziri Mkuu ili wananchi waishi kwa amani

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here