25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JITENGE NA MATATIZO USONGE MBELE KIMAFANIKIO

Na ATHUMANI MOHAMED

KATIKA harakati za kusaka mafanikio utulivu wa akili ni kitu cha msingi sana. Ikiwa utakosa utulivu wa akili ni wazi kuwa hutaweza kutia bidii katika mambo yatakayokufanikisha.

Inaweza kuonekana kama ni jambo gumu, lakini ndugu zangu ukweli ni kwamba hakuna jambo linalotokea kwa bahati mbaya, kama yapo ni machache sana.

Mathalani wanasema ajali haina kinga, kwamba hutokea kwa bahati mbaya tu bila taarifa. Lakini ukweli ni kwamba asilimia kubwa za ajali zina kinga.

Huwezi kuendesha mwendo mkali, halafu ukapata ajali ukasema eti ajali haina kinga. Utakuwa unashangaza sana. Binadamu tumekuwa tukiishi kwa mazoea na kukiri matatizo jambo ambalo si zuri kwa hakika.

Ikiwa gari lako utakuwa unalipeleka garage kila wakati kukaguliwa ni wazi kuwa likipata hitilafu ndogo za kawaida kabla tatizo halijawa kubwa utafahamu na kutafuta namna ya kulitengeneza na hivyo kukuepusha na ajali.

Ajali za bahati mbaya ni zile za kugongwa, kuangukiwa na vitu vizito n.k huo ndiyo ukweli ambao wengi wataukataa. Tukiishi kwa kufuata misingi, haya mambo ya kusingizia bahati mbaya yatapungua kama siyo kuondoka kabisa katika maisha yetu.

Wakati fulani kwenye maisha mtu anaweza kujikuta akishindwa kufanikiwa au kuchelewa au kupatwa na misukosuko isiyo ya kawaida ambayo itamyumbisha kumbe ni kwa kujitakia mwenyewe.

Katika mada hii lengo ni kukumbushana mambo ya msingi ya kuzingatia ambayo unapaswa kujiweka nayo mbali ili usiwe na vikwazo vitakavyokuvuta shati kuelekea kwenye mafanikio.

 

ZINGATIA KANUNI ZA AFYA

Katika mambo ya msingi zaidi kuzingatia katika maisha ni pamoja na kanuni za afya. Zipo nyingi lakini naamini nyingi zinajulikana – zile za jumla zaidi. Lakini hata mtindo wa maisha unahusisha moja kwa moja afya zetu.

Mathalani suala la lishe ni muhimu sana lakini wengi wanaonekana kuchukulia kama jambo la kawaida. Kuna watu wanafanya suala la mlo kama la dharura tu.

Je, unaangalia unachokula? Kina faida au hasara mwilini mwako? Achana na milo ya kujaza tumbo. Ni vizuri kula vyakula vyenye virutubisho vyote.

Vyakula hivyo ni pamoja na vile visivyokobolewa, matunda, mboga za majani za kutosha na maji ya kunywa ya kutosha. Unapaswa kula matunda angalau katika mlo mmoja kila siku na mboga za majani angalau kwa milio mmoja wa kila siku.

Unapaswa kuhakikisha unakunywa maji angalau robo lita kabla ya mlo wako na nusu lita kila baada ya saa moja ya kila mlo, kipimo cha maji cha kutwa kisiwe chini ya lita tatu.

Unapaswa kukaa mbali na vyakula vyenye mafuta mengi. Je, wewe unayekula chipsi mayai kama mlo wako mkuu kila siku unajua unachokitengeneza? Kesho ukizidiwa na presha utamlaumu nani?

Wewe ambaye sehemu ndogo tu unatumia gari, huna mazoezi, matarajio yako ni nini? Ndugu zangu, tunapaswa kufanya mazoezi  angalau nusu saa kila siku. Wapo watu hawana muda wa mazoezi kabisa, lakini wana muda wa kunywa bia na nyama choma.

Wanaumuka matumbo wanadhani ndiyo afya. Siyo kweli ni kujidanganya tu. Zingatia kanuni za afya maana ukianza kuumwa, utapoteza furaha na ukipoteza furaha hutaweza kufukuzana na maisha tena.

Wiki ijayo tutamalizia mada yetu, USIKOSE!

Wako katika mafanikio, Athumani Mohamed. Wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles