NA GEORGE KAYALA
MWIGIZAJI Susan Humba ‘Natasha’ amewataka wenye makampuni ya uandaaji wa filamu za bongo kuwatumia watoto wenye vipaji ambao wana ulemavu wa viungo.
Natasha alitoa kauli hiyo kwa watoto hao wenye ulemavu wa viungo wanaosoma Shule ya Sekondari Jangwani, jijini Dar es Salaam, baada ya kuonyesha uwezo wao wa kuigiza mbele yake.
Wanafunzi hao walionesha vipaji vyao mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati wa uzinduzi wa shirika lisilo la kiserikali la Save Vulnerable Foundation (SVF), linalojishughulisha na kusaidia watoto wenye ulemavu mashuleni, uliofanyika shuleni hapo.
“Nimeona vijana hawa wana vipaji vya uigizaji, hivyo nitaangalia namna ya kuwasaidia, lakini pia nawataka wale wanaojihusisha na masuala ya filamu waje wawachukue kwa ajili ya kuwatumia kwenye sinema zao, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuwapa ajira kwa kutumia sanaa hiyo ya maigizo,” alisema msanii huyo.