Na JUDITH NYANGE-GEITA
WAKAZI wa Mtaa wa Nyantorotoro B, mkoani Geita, wameiomba Serikali kuifuatilia ahadi waliyopewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kutimiza ahadi yake ya kufikisha maji mtaani kwao, kwa kuwa yamekuwa yakipatikana umbali wa kilomita sita katika kijiji jirani.
Akizungumza na MTANZANIA juzi, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyantororo B, Fikiri Sylvester, alisema walikuwa wakiutegemea mradi wa maji wa GGM, ambao ulisambaza bomba la kutoa maji kwa kaya mbili tu, ambayo yamekuwa yakitoka kidogo, hivyo kusababisha adha kubwa ya maji.
Alisema kutokana na maji hayo ya bomba yaliyosambazwa na mgodi kutotoka, wakati mwingine wanawake wamekuwa wakilazimika kuyafuata umbali wa kilomita sita katika Kijiji cha Mkolani, ambako wamepokea malalamiko ya wanawake kubakwa njiani.
Mmoja wa manusura wa tukio hilo, Njile Makungu, alisema wanalazimika kila siku kuamka saa 8 usiku na kurudi saa tatu asubuhi na maji au bila kupata maji, ambapo hukutana na vijana wanaovuta bangi ambao huwakimbiza na kutaka kuwabaka.
“Kwa Juni, mwaka huu pekee walifika wanawake sita ofisini na kutoa malalamiko ya kubakwa pindi walipokwenda kuteka maji, uongozi wa mtaa tuliitisha mkutano wa hadhara wa wananchi wote na kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi kwa ajili ya kufanya doria wakati wanawake wanapoamka kwenda kuteka maji pamoja na kutoa taarifa kwa ofisa mtendaji wa mtaa, kwa sasa tatizo hilo limepungua,” alisema Sylvester.
Alisema licha ya kuchukua hatua za dharura kwa kuweka ulinzi njiani, bado serikali inapaswa kufuatilia mradi huo wa maji wa mwekezaji na kuhakikisha unakuwa wenye ufanisi mkubwa kwao kwa kutoa maji yatakayotosheleza mahitaji yao, ikiwa ni pamoja na kusambaza bomba kwa kaya mbili.
Akizungumzia hali hiyo, Mhandisi Mkuu wa Maji wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Gasper Shoo, alisema suala la maji bado ni changamoto sana, kwani ni asilimia 17 tu ya wakazi wa mji huo ndio wanaopata maji na kuwataka kungojea mradi mkubwa ukamilike.
Alisema mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa na mgodi huo wa GGM kwa kushirikiana na serikali kwa gharama ya Sh bilioni 12.7, utasambaza maji kwa baadhi ya maeneo ya mji huo na yale yaliyobaki yanatarajiwa kutapatiwa maji kupitia Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Ziwa Victoria awamu ya pili (LVWATSAN-II), unaotarajia kuanza Agosti, mwaka huu.