26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CCM AZUA TAFRANI

Wabunge wa Viti Maalumu wa CCM, Rose Tweve (kushoto) na Taska Mbogo (kulia), wakimzuia mbunge mwenzao Juliana Shonza, baada ya kuzozana na wabunge wa upinzani wakati wakielekea kwenye mkutano na waandishi wa habari bungeni Dodoma jana.

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

MBUNGE wa Viti Maalumu, Juliana Shonza (CCM), amenusurika kipigo kutoka kwa wabunge wenzake wa upinzani baada ya kudaiwa kutoa lugha ya kuudhi.

Wakati wa patashika hiyo inadaiwa kuwa chanzo chake ni kauli ya Shonza aliyedaiwa kutamba mbele ya wabunge hao kuwa atahakikisha Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) harudi bungeni.

Tukio hilo lilitokea jana katika viwanja vya Bunge, wakati Shoza alipokutana na wabunge wa upinzani waliokuwa wakielekea katika ukumbi kwa ajili ya mkutano na wanahabari.

Shonza ambaye alikuwa ameongozana na Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Tweve (CCM) alidaiwa kueleza kwamba atawasilisha maoni bungeni ili Mdee aendelee kusota nje ya Bunge kutokana na alichodai matendo yake anayofanya hayaendani na hadhi ya wabunge.

Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema), ambaye alikuwa pembeni alimtaka Shonza kuacha roho mbaya na kumwogopa Mungu kwani hata Mdee akikaa nje ya Bunge hatofaidika na chochote.

Mbunge huyo alimweleza Shonza kuacha roho mbaya huku akimuhoji ni kwanini anafurahia matatizo ya mwanamke mwenzake.

“Wewe ni mwanamke acha roho mbaya unafurahia vipi mwenzako akipata matatizo? Kukaa kwake nje hakuwezi kukusaidia kitu ila malipo ni hapa hapa duniani,” alisema Kiwanga.

Kauli hiyo ilionekana kumkera Shonza ambaye alitaka kukunjana na mbunge huyo.

Hatua hiyo ilimfanya Shonza kuanza kujibu ndipo baadhi ya wabunge wa Chadema waliokuwa jirani akiwemo Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekule, wakaanza kumtaka awe na hekima kwa kuangalia umri wa mbunge aliyekuwa akimtolea maneno machafu.

Licha ya kukatazwa Shonza hakutaka kuelewa na badala yake aliendelea kuzungumza, ndipo Tweve pamoja na mwenzake Taska Mbogo wa CCM, walipolazimika kumvuta lakini Shonza aliwataka wenzake wamuache ili apambane na wabunge hao wa upinzani.

“Niacheni kama wanataka kunipiga tuone, niacheni niacheni,” alisikika Shonza akijibu kwa hasira huku akivutwa na wabunge wenzake wa CCM.

Hata hivyo Gekul aliwasihi wabunge hao wa CCM kumfunza adabu Shonza ili ajue kuheshimu watu anaozungunza nao na apunguze jazba badala ya kugombana na watu wazima.

“Mheshimuwa Vulu (Zainab) mfunzeni adabu huyu binti ana matatizo makubwa haiwezekani anajibishana na watu wazima huku akitaka kupigana nao ni aibu mnatuambia sisi tuambizane ukweli lakini huyu binti mnamuangalia anaharibikiwa ,” alisema Gekul.

Baadae ilielezwa kuwa Shonza alikwenda Polisi kufungua jalada la malalamiko dhidi ya wabunge wa Chadema.

Akizungumza na MTANZANIA jana Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Ernest Kimola alithibitisha Shonza kufungua kesi ya shambulio la kudhuru mwili.

Alisema mbunge huyo alidai kupigwa na wabunge wa Chadema katika viwanja vya Bunge.

Spika Ndugai

Hata hivyo wakati akiahirisha Bunge jana jioni Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema Shonza alikwenda ofisini kwake na kulalamikia hatua ya wabunge wa Chadema kutaka kumpiga.

Kutokana na malalamiko yake hayo, alisema alimwelekeza mbunge huyo kwenda polisi ili haki yake iweze kupatikana.

“Suala hili ni la kijinai hivyo naeleza wabunge wanapokuwa hata katika viwanja vya bunge hawana kinga dhidi ya makosa ya kijinai hivyo napenda kuwajulisha kuwa mheshimiwa Shonza ameniomba na nimempa kibali kulifikisha suala hilo polisi,’’ alisema.

Spika aliwataja wabunge wanaodaiwa kutaka kumpiga  kwa majina na majimbo yao kwenye mabano kuwa ni Saed Kubenea (Ubungo), Suzan Kiwanga (Mlimba), Frank Mwakajoka (Tunduma), Joseph Selasin (Rombo), Paulina Gekul (Babati Mjini), Cecilia Pareso na Devotha Minja (viti maalum).

Mwandishi atiwa kashkash

Wakati hayo yakiendelea baadhi ya waandishi waliokuwepo pembeni akiwemo mpigapicha wa gazeti hili, Silvan Kiwale alijikuta akikamatwa kwa muda na maofisa usalama wa Bunge kwa kumtaka kutozitumia picha alizopiga za wabunge hao.

Kutokana na hali hiyo maofisa hao walimchukua mpigapicha  huyo na kwenda naye katika ofisi ya Katibu wa Bunge, huku wakitaka wapewe picha za tukio hilo.

Mbali na hilo pia walimuhoji ni kwa nini amepiga picha hizo sambamba na kuzituma kwenye chombo chake cha habari licha ya katazo lao la kumtaka asifanye hivyo.

Baada ya muda maofisa hao walitaka wapewe picha hizo ndipo mpigapicha huyo alipowapa na kumwachia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles