MANJI ADAIWA KUKAMATWA TENA

0
632
Yussuf Manji.
Yussuf Manji.

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linadaiwa kumshikilia aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yussuf Manji.

Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi ziliambia MTANZANIA kuwa Manji pamoja na ofisa wake mmoja wanashikiliwa tangu Ijumaa ya Juni 30, mwaka huu ambapo inadaiwa katika moja ya ghala la kampuni yake lilihifadhi sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mfanyabishara huyo Casto Ngogo (35), ambaye anatajwa kukamatwa na Manji, alipandishwa kizimbani Juni 21, mwaka huu  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na sare za jeshi hilo zikiwmao suruali 5,000.

Inadaiwa kuwa Juni 15, maeneo ya Bandari Kavu ya Galco, Chang’ombe, Temeke, Dar es Salaam, Ngogo alikutwa na suruali hizo 5,000 za JWTZ kwenye kontena namba PCIU 82851 (5) zikiwa na thamani ya Sh milioni 59 mali ya Serikali bila kibali.

Hatua ya kukamatwa kwa Manji inatajwa kuwa ni sehemu ya kusaidia maelezo katika kesi hiyo ambapo anahusishwa kwa maghala yake kuhifadhi sare hizo za jeshi.

Gazeti hili lilipomtafuta Msemaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mussa Misalaba, alisema yupo nje ya ofisi ambapo alimtaka mwandisi kuwasiliana na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Takukuru, Alex Mfungo.

Alipotafutwa Mfungo kuhusu suala hilo naye alimtaka mwandishi kumtafuta tena msemaji wa Takukuru kwani ndiye anayehusika na kuzungumzia suala hilo.

“Mtafute msemaji ndiye anahusika na mambo yote mimi siwezi kuongea kwani tutakuwa tunaingiliana majukumu,” alisema mkurugenzi huyo.

Kutokana na hali hiyo gazeti hili lilirudi tena kwa Misalaba, ambapo alisema ni kweli Mkurugenzi huyo hawezi kuzungumzia suala hilo huku akimtaka mwandishi kuwa na subira kuhusu suala hilo la Manji.

“Kesho (leo) nitawatafuta wahusika na kisha nitakuambia,” alisema Misalaba.

Pamoja na hali hiyo alipitafutwa Mkurugenzi wa Takukuru, Valentino Mlowola, alisema kuwa hana taarifa za kukamtwa kwa Manji kwani yupo nje ya ofisi huku akimtaka tena mwandishi kumtafuta Msemaji wa Takukuru.

Kutokana na mzunguko huo wa Takukuru MTANZANIA ilimtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, ambapo simu yake haikupokewa wala hakujibu  ujumbe mfupi wa simu.

Inadaiwa kuwa Manji ambaye kwa sasa yupo mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi, anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Februari 9, mwaka huu Manji alikamatwa  na Polisi baada ya kujisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam,  baada ya kutajwa katika orodha ya watu 65 wanaodaiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here