26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATOA ONYO KWA WANASIASA

Na ELIZABETH HOMBO

Ni onyo la mwisho. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais Dk. John Magufuli kuwataka wanasiasa kuchunga midomo yao kwa kuwatetea masheikh waliopo mahabusu.

Rais Dk. Magufuli ametoa onyo hilo ikiwa ni siku chache baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI) kumhoji Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutokana na kauli zake zinazodaiwa kuwa za uchochezi kwa kutaka masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara Zanzibar (Jumuki) maarufu ‘Uamsho’ waachiwe.

Mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo    wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam jana   ingawa hakutaja moja kwa moja jina la mwanasiasa yeyote.

Rais   alilitaka Jeshi la Polisi kushughulika na wanasiasa waropokaji wasaidie kwa upelelezi wakiwa rumande.

“Nataka polisi mfanye kazi zenu … hawa wanaoropokaropoka waisaidie polisi kupeleleza. Msiogope cha sura, mwendo wake awe na speed ya kukimbia, ya polepole, atayaeleza vizuri akiwa pale lockup.

“Niwaombe wanasiasa ambao wameshindwa ku-control (kudhibiti)  midomo yao…saa nyingine wanazungumza hata mambo wasiyoyajua, anashindwa kuelewa Marekani wale walioshtakiwa walikaa katika gereza la Gwantenamo…

“Kuna watu wamekufa zaidi ya 35, askari 15 na wanaohusika ni pamoja na hao sasa mtu anatoka pale anazungumza kuwa wamekaa mno. Unaweza kuona huyu lazima anahusika kwa njia moja au nyingine, wasitufanye tufike huko kwa sababu wataumia.

“Wajifunze kufunga midomo yao wakati Serikali inafanya kazi yake. Kuna mambo makubwa katika nchi hii tunayoshughulika nayo.

“Utakuta mnashughulikia rasilimali zinapoibwa, utakuta mtu anapinga hadharani kwa sababu amepewa vijinsenti. Hujasimama hata siku moja kulaani watu wanaokufa huko, tena ambao hawana hatia.

“Wanavamia mtu ambaye hana silaha, si waje wapambane na askari walio na bunduki kama wao ni wanaume kweli. Unavamia mzee hana hata silaha ametoka shambani anapigwa risasi.

“Halafu unatoka mwanasiasa kwa kutaka sifa za siasa unasimama hadharani… huyu mtu aachiwe na hujawahi kulaani wanaokufa na bahati mbaya wanaokufa ni wa chama kimoja tu fulani,” alisema Rais Dk. Magufuli

Alisema anazungumza hayo kwa sababu amepewa nafasi ya kuongoza Taifa kwa miaka mitano kama Rais mwenye jukumu la kulinda pia usalama wa Watanzania wote.

“Nazungumza haya kwa sababu nimepewa nafasi yangu ya  miaka mitano kama Rais, lakini jukumu langu lingine ni kulinda usalama wa Watanzania.

“Maendeleo haya tunayoshughulikia yanakuja sababu ya usalama na nchi ikikosa usalama hakuna maendeleo na hakuna mwekezaji atakayeweza kuja hapa.

“…juzi zimekamatwa sare za jeshi 5,000 wanaohusika katika upelelezi ni pamoja na hao halafu unatoka hadharani unasema waachiwe.

“Maana yake na wewe ulihusika kuleta hizo uniform … watch out, nadhani wamenielewa,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alihojiwa kwa saa nne katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI),Dar es Salaam,  akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi.

Juni 24 mwaka huu, inadaiwa Lowassa alitoa maneno ya uchochezi wakati wa futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Taarifa za ndani zilieleza kuwa katika mahojiano hayo, Lowassa aliwekewa mikanda ya video mbalimbali kuhusu matamshi aliyotoa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 yanayohusu ahadi yake ya kuwatoa kizuini masheikh wa Jumuiya ya Mihadhara (Uamsho).

Baada ya kuwekewa video hizo alitakiwa kueleza kwa kina kauli zake hizo zilikuwa na maana gani kwa usalama wa nchi.

Pamoja na hali hiyo, inaelezwa kuwa bado Lowassa alisimamia msimamo wake akisisitiza hakuna sehemu aliyotamka uchochezi.

“Nilikwenda polisi na kuhojiwa juu ya hotuba niliyoitoa kwa Waitara wakati wa futari, kuna watu wameitafsiri kwamba ni uchochezi. Polisi wana shaka hivyo wana haki ya kunihoji.

“Niwahakikishie wanachama wenzangu hatujafanya kosa lolote, tulikuwa tunatekeleza sera ya chama chetu, wakae salama wasubiri taratibu zifuatwe,” alisema Lowassa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles