…ASHTUKIA MCHEZO MCHAFU VICHWA VYA TRENI BANDARI

0
789

Na ELIZABETH HOMBO

Rais Dk. John Magufuli amewaumbua wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Dar es Salaam (TPA) baada kufichua siri ya kupokea vichwa vya treni 15 ambavyo havina mkataba wowote.

Amesema ni wazi mchezo huo umefanyika kwa sababu Shirika la Reli Tanzania (TRL) lilieleza bayana kwamba halijaagiza wala kusaini mkataba wowote kuhusiana na vichwa hivyo.

Rais Magufuli alifichua siri hiyo jana wakati akizindua mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam   utakaogharimu Sh bilioni 926.2.

“TPA muangalie security (usalama) ya hapa … juzi juzi vimeshushwa vichwa vya mabehewa na havina wenyewe. Hamjanieleza lakini mimi nataka Watanzania wajue.

“Vichwa 15…wamefanya mission yao na havihitajiki TRL, wanasema hawajaagiza wala hakuna document (nyaraka) yoyote waliyosaini ya kusema wanahitaji lakini vimekuja vikateremshwa hapa wala hamuulizi vimetoka wapi.

“Walivyomaliza kuteremsha TPA ndiyo mkaanza kuuliza wakati meli ilishaondoka na vichwa venyewe inasemekana ni vibovu. Ni lazima hapa kulikuwa kuna mchezo na inawezekana rushwa ilikuwa inatembea.

“Nina uhakika Wizara mtakaa.  Inawezekanaje vichwa vinatereshwa bila kujua vinaenda wapi.

“Siku nyingine watateremsha hata vifaru na mkavipokea bila kuuliza vinaenda wapi au kontena la sumu ni kwa sababu hakuna ‘coordination’ nzuri.

“Sijui TPA na wizara mtayafanyia nini labda mtayasaga yawe maskrepa. Najua hili hamtaki watu wajue sasa mimi nalisema hadharani ili Watanzania wajue na ubovu wa hapa,”alisema Rais Dk. Magufuli

Alivitaka vyombo vya dola   kuchunguza   inakuwaje vitu viteremshwe bila mkataba.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema kuna kampuni moja ambayo hakuitaja   jina,   imekuwa ikifanya mchezo wa kukwepa kodi.

“Kuna dalili fulani fulani za ukwepaji wa kodi tunaambiwa. Mshughulikie ukwepaji huu TPA, TRA na wizara, kuna kampuni moja jina nalihifadhi hapa inakwepa.

“Ilikwepa siku za nyuma ikajifuta kwamba si kampuni ikaanzisha kampuni nyingine… kuna mchezo huo.  Nalizungumza hili ili wahusika wote muanze kulishughulikia,”alisema Rais Magufuli.

TPA YAFAFANUA

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya hotuba hiyo ya Rais, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),  Deusdedit Kakoko, alisema vichwa hivyo vya mabehewa vilitengenezwa  siku zilizopita na vingine vikatangulia na kuanza kutumika lakini mchakato wa ununuzi ulikuwa na walakini.

Alisema baadaye Serikali haikupenda kuendelea na awamu ya pili ya vichwa 11 vilivyokuwa vimebakia lakini Kampuni ya Khomaz ya Afrika Kusini ilikuwa imeshamaliza kutengeneza.

“TRL hawakuvitaka na sisi hatukugundua kama kuna mgogoro kati ya TRL na Kampuni ya Khomaz inayotengeneza.  Tulivyowaambiwa TRL waje wavichukue  wakasema hawavitambui.

“Si sisi TPA wenye makosa na hata TRL nao hawakujua aliyeleta na mwenye meli ambayo inaitwa MESSINA.

“Kuhusu kodi bado hatujajua kama wamelipana na TRA kwa sababu na katazo hili huwezi kupokea wala kulipia,”alisema  Kakoko.

MRADI

Awali akizungumzia  mradi huo, Rais Magufuli alisema kukamilika kwake kutaifanya Tanzania  kuwa  kitovu cha uchumi kwa sababu itahudumia na nchi nyingine.

Rais alisema uboreshaji huo utawezesha bandari hiyo kuhudumia meli kubwa na kuongeza   mizigo..

Mradi huo ulikuwa umepangwa kukamilika ndani ya miezi 36, lakini Rais Magufuli aliitaka Kampuni ya China ya Harbour Constructioni Engineering (CHCE) ambayo ndiyo inasimamia mradi huo, kuukamilisha ndani ya miezi 28.

“Mradi huu utatekelezwa kwa awamu mbili kuanzia gati moja mpaka saba na gati ya kuhudumia magari inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 28 badala ya 36.

“Fedha zipo kwa nini wakae mpaka miezi 36 wanasubiri nini ili gharama nayo ipungue. Huyu mkandarasi ana wajibu wa kufanya kazi usiku na mchana,”alisema.

Alisema mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 421 ( Sh bilioni 926.2).

“Kutokana na mkataba wa awali, Tanzania imetoa dola za Marekani milioni  63.4, Benki ya Dunia imetoa mkopo wa dola za Marekani milioni 345 huku Serikali ya Uingereza kupitia idara yake ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID) ikitoa dola za Marekani milioni 12.4,”alisema.

Kazi ya ujenzi, upanuzi na ukarabati huo zitafanyika katika gati namba moja hadi saba ambazo zinaendeshwa na TPA.

Pia itaongeza kina cha bahari kwa kuongeza urefu kutoka wastani wa mita 12 hadi kufikia mita 15.5 na kukarabati miundombinu wezeshi ya bandari.

Mbali na viongozi wengine wa taifa, hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi wa Uingereza  nchini, Sarah Cooke na Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bella Bird.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa   Tanzania ambaye pia anasimamia Malawi, Burundi na Somalia, Bella Bird, alisema ujenzi wa bandari hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania na nchi jirani.

“Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu   kwa uchumi wa Tanzania na nchi jirani. Kukuza uwezo wake wa kufanya shughuli na kuinua biashara na kutengeneza ajira katika ukanda huu,” alisema Bird.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here