MARKUS MPANGALA NA MASHIRIKA YA HABARI,
RAIS mstaafu Barrack Obama alikuwa na watu wanne aliowaamini sana; David Plouffe, David Axelrod, Rahm Emmanuel na Valerie Jarrett.
Katika kipindi cha ‘The Axe Files’, Obama amewahi kukiri kuwa marafiki zake hawajawahi kumwita rais badala yake wanamwita Barrack au Barry.
Kila rais anapoingia madarakani, kuna watu wake wa karibu anaowaamini katika utendaji wa kazi.
Hilo ndilo linalotokea kwa Jared Kushner (36), ambaye ni mkwe wa Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump aliyeoa binti yake mkubwa aitwaye Ivanka.
Yapo mambo ya kujiuliza ili kufahamu nafasi ya Kushner katika utawala wa Trump.
Anafanya mambo gani ambayo yanasababisha si tu kuwa mtu wa karibu wa rais huyo, bali pia kuzua mijadala?
Je, kitu gani anakifanya ambacho Rais Trump hawezi na hata kulazimika kumlipa kwa fedha zake binafsi?
Kushner ambaye Trump alimteua kuwa mshauri wake mwandamizi, jina lake linaonekana kukua siku hadi siku likielezwa kutajwa zaidi ndani ya Ikulu ya Marekani.
Mtu huyu amepewa majukumu makubwa yakiwamo yale ambayo kiutamaduni yalikuwa yakifanywa na ama Mkuu wa Majeshi ambaye ni mshauri wa masuala ya kijeshi kwa rais au mtu ambaye kwa Tanzania tungemwita Katibu Mkuu Kiongozi.
Shirika la Utangazaji la CNN, limemwelezea Kushner kama mtu ambaye ana nguvu kubwa ndani ya Ikulu ya Marekani.
Kwamba licha ya kutokuwa na uzoefu katika masuala ya kidiplomasia, lakini amekuwa kiungo muhimu kati ya Marekani na masuala ya mahusiano ya kimataifa, akionekana katika kila jambo kubwa linalohusu uongozi.
Tukio la hivi karibuni ambalo limezidisha mjadala ni lile ambalo liliripotiwa na CNN, kuhusu ziara yake ya kutembelea Iraq kupata taarifa fupi ya kampeni ya kijeshi dhidi ya ISIS.
CNN imeeleza kuwa jambo hilo huko nyuma halikupaswa kufanywa na mtu kama Kushner.
Kwa mujibu wa CNN, ziara hiyo ilipaswa kufanywa na Mkuu wa Majeshi.
Jambo hilo limetafsiriwa kuwa ushawishi wa Kushner ndani ya Serikali ya baba mkwe wake umeongezeka katika kila eneo.
Wachambuzi nchini Marekani wanasema nguvu ya Kushner ilianza kuonekana mapema kutokana na kitendo cha kuchunguzwa kwake na Mwendesha Mashtaka Rober Mueller iwapo alishirikiana na Serikali ya Urusi kumsaidia Trump kupata ushindi katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana.
Ni nani huyu Jared Kushner?
Kushner alizaliwa Januari 10, mwaka 1981 huko Livingston mjini New Jersey, Marekani. Ni mtoto wa Charles Kushner na mama yake ni Seryl Kushner.
Kijana huyu ana asili ya Kiyahudi kutoka Israel. Ndugu zake ni Joshua, Nicole na Dara Kushner na alihitimu Chuo Kikuu cha New York.
Baba yake ni mfanyabiashara mkubwa wa majengo. Wanamiliki Kampuni ya Kushner Company.
Pia ni mmiliki wa Kampuni ya Observer Media Group ambayo inachapisha gazeti la New York Observer. Hata hivyo Januari mwaka huu alijiuzulu na nafasi yake ikachukuliwa na shemeji yake, Joseph Meyer ambaye sasa ndiye anaongoza kampuni hiyo.
Inaelezwa kuwa gazeti hilo limewahi kulalamikiwa na washindani wake kibiashara, kwani analitumia kama sehemu ya kueneza propaganda za biashara za majengo.
Baba yake amewahi kufungwa jela kwa miaka miwili kwa kosa la ukwepaji wa kodi na uvunjaji wa sheria za uchaguzi mwaka 2004.
Mtu na mkwewe
Inafahamika kuwa Kushner ni mkwe wa Trump kutokana na kumuoa binti yake aitwaye Ivanka. Walifunga ndoa mwaka 2009 baada ya kudumu kwenye uhusiano kwa miaka minne.
Ili kutimiza kigezo cha kufunga ndoa, ilimlazimu Ivanka kubadili dini na kujiunga na Uyahudi katika Kanisa la Orthodox wanaloabudu Wayahudi kokote wanakoishi duniani.
Kushner ni mtu wa namna gani?
Mojawapo ya sifa zinazotajwa kwa Kushner ni upole, lakini ni mtu makini.
Mara nyingi amekuwa nyuma ya Rais Trump katika tafrija na ziara mbalimbali za kiserikali, akiwa kimya bila kuzungumza na watu wanaojumuika naye.
Nafasi yake ni ipi kwa Trump?
Kwa sasa Kushner ni mshauri mwandamizi wa Ikulu. Ni msimamizi wa mazungumzo ya kusaka amani Mashariki ya Kati baina ya Israel na Palestina.
Vilevile ni msimamizi wa uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Serikali ya Marekani na Canada, Mexico na China.
Kwa hiyo matamko au uamuzi unaochukuliwa na Rais Trump dhidi ya mataifa hayo, umekuwa ukibarikiwa na Kushner mwenye kuwajibika kumshauri na kumwelekeza cha kufanya.
Kwa mujibu wa Rais Trump, Kushner anapenda sana siasa kuliko biashara zake za majengo.
Msiri wa Rais Trump
Kushner alianza kushirikiana na Rais Trump tangu akiwa kwenye harakati za kampeni.
Ni yeye ndiye alianzisha kampeni za kumchagua Trump kupitia mitandao ya kijamii ya ‘Project Alamo’.
Baadaye alimteua kuwa meneja wa kampeni zake za urais. Vilevile ndiye aliyemwandikia hotuba Trump na kumsaidia kuunda safu ya uongozi wa Serikali mara baada ya kutangazwa mshindi.
Kushner alichukua nafasi hiyo baada ya Corey Lewandowski kufukuzwa kama Meneja wa Kampeni za Trump. Yeye ndiye alikuwa mpanga mikakati ya ushindi.
Anatajwa kuwa ndio mtu anayemsaidia zaidi Trump katika uongozi wake kwa sasa serikalini.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Google, Erick Schmidt, aliiambia Televisheni ya CBS kuwa Kushner ameshangaza wengi tangu mwanzoni, hususani kutokana na hatua ya kuingia kwenye kampeni na kuwa sehemu ya Serikali inayoongozwa na Rais Trump.
Pia Kushner anatajwa kuhusika kufukuzwa kazi kwa Chris Christie aliyekuwa msimamizi wa kupanga safu ya uongozi wa Serikali baada ya ushindi wa urais.
Tim Obrien ambaye ndiye mwandishi wa wasifu wa Trump, anasema kiongozi huyo anamwamini sana Kushner kwa sababu ni sehemu ya familia yake.
“Inaonyesha Trump hawaamini watu wengine kama sio sehemu ya familia yao,” alisema Tim Obrien alipozungumza na Televisheni ya CBS
Spika wa zamani wa Bunge kutoka Chama cha Republican, Newt Gingrich anasema Kushner anayajua malengo ya Rais Trump ndiyo maana anaaminika.
Taarifa za ndani zinasema kuwa ni Kushner ndiye alimshauri Trump amfukuze kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), James Comey.
Wakati Rais Trump akitangaza uamuzi wa Serikali kujiondoa katika mkataba wa Paris kuhusu tabianchi mwezi uliopita, inaelezwa haukumfurahisha bintiye Ivanka, lakini Kushner alifahamu na kuwa sehemu ya uamuzi uliochukuliwa na rais huyo wa Marekani.
Kwa nini Kushner anachunguzwa?
Tangu alipotangazwa mshindi wa kiti cha urais, Trump ametuhumiwa kupata ushindi huo kwa msaada wa Urusi.
Mara kadhaa amekanusha jambo hilo, lakini sasa limefika mahali pagumu. Hata hivyo jina la Kushner limejitokeza katikati ya kadhia hiyo akidaiwa kuwa mtu ‘katikati’ kati ya Urusi na iliyokuwa timu ya kampeni ya Trump. Kwamba yeye ndiye alikuwa mpanga ‘madili’.
Kwa mujibu wa gazeti la The Washington Post, Kushner alikutana na Balozi wa Urusi, Sergey Kslyak Desemba mwaka jana.
Inadaiwa balozi huyo alimshawishi kuanzisha mawasiliano binafsi na Serikali ya Urusi kwa kutumia vifaa vya nchi hiyo.
Uhusiano na Israel
Kwa mujibu wa jarida la Politico, Kushner ana uhusiano wa karibu na chama cha Wayahudi kijulikanacho kama Chabad-Lubavotch huko Urusi.
Kutokana na asili yake ya Israel kisha kuteuliwa kama msimamizi wa kutafuta amani baina ya taifa hilo na Palestina, ni jambo linalozua mjadala kote nchini Marekani.
Wachambuzi wanaeleza kuwa kwa kutambua nafasi ya Kushner ndani ya Israel, baadhi ya nchi ambazo zimekuwa zikitaka kunufaika na misaada ya Marekani zimetumia mwanya huo kuwa karibu na taifa hilo la Kiyahudi.
Hadi sasa Wamarekani wengi wanaamini Serikali ya Trump inasimamiwa na Kushner kutokana na matendo, uamuzi na hatua zinazochukuliwa na kwamba uteuzi wake haujavunja sheria yeyote ya Marekani.