23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

LIPUMBA AMWEKEA MTEGO MWINGINE MAALIM SEIF

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa Kamati ya Maadili ya chama hicho. Kulia ni Katibu wa Kamati ya Maarifa ya chama hicho, Khalifa Suleiman Khalifa na Mkurugenzi wa Mipango na Uchumi wa chama hicho, Mneke Jafar. Picha na John Dande

Na AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF) upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, umezindua Kamati ya Maadili na Nidhamu ambayo pamoja na mambo mengine imepewa jukumu la kuchunguza mienendo ya wanachama, kuwaita na kuwahoji wote walioonyesha utovu wa nidhamu, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hii si mara ya kwanza kwa wanachama na viongozi wa chama hicho kuitwa mbele ya kamati hiyo inayoundwa na wajumbe wanane kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ibara ya 99.

Itakumbukwa uamuzi uliowahi kutolewa na kamati hiyo na kutikisa ni ule wa Januari 2012 wa kumfukuza uanachama aliyekuwa Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake.

Akizungumza jana katika Ofisi Kuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam, Profesa Lipumba alisema kamati hiyo inaanza kufanya kazi mara tu baada ya kuzinduliwa na kwa kuanza kumuhoji Maalim Seif ambaye ana tuhuma sita zinazomkabili.

Alisema Maalim Seif na wanachama wengine akiwamo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, wabunge na madiwani, wanadaiwa kwenda kinyume na taratibu za chama hicho na kwamba kamati itawahoji kwa kutekeleza maelekezo ya  wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

“Tulikuwa na mgogoro ndani ya chama, katika mgogoro huo kuna watu wamevunja maadili na nidhamu ya chama, Baraza Kuu limeiagiza Kamati ya Nidhamu kuhoji baadhi ya viongozi na wanachama, wa kwanza na muhimu sana katika hili ni Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema Maalim Seif anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo na kujitetea kwa makosa mbalimbali aliyonayo ikiwamo  kushindwa kufika katika ofisi za chama kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, Katibu Mkuu huyo pia anatuhumiwa kukaidi maagizo aliyokuwa akipewa na mwenyekiti yaliyomtaka kuitisha vikao halali vya chama, pia anatuhumiwa kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kukihujumu chama chao.

“Katika majukumu aliyopewa ni kufuata maelekezo ya mwenyekiti, lakini yeye amekuwa mkaidi, ameshirikiana na viongozi wa Chadema kuihujumu CUF, Chadema wamefikia hatua wanakisemea chama, huko ni kukidhalilisha chama, hususani Tanzania Bara. Aseme mbele ya kamati kwa nini amefanya hivyo,” alisema Profesa Lipumba.

Alitaja tuhuma nyingine inayomkabili Maalim Seif kuwa ni kuwazuia wawakilishi, wabunge na masheha walioshinda katika Uchaguzi Mkuu mwaka juzi kwenda mahakamani kufungua kesi  wakiwa na vyeti vyao vya ushindi ili kutetea viti hivyo ambavyo kikatiba ukishatangazwa hupaswi kutenguliwa.

“Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, Baraza Kuu lilifanya uamuzi wa kuwataka wawakilishi, masheha wote wa Zanzibar waliopata ushindi waende kufungua kesi mahakamani wakiwa na vyeti vyao kwakuwa walishatangazwa washindi.

“Kulingana na majadiliano ya wajumbe na ushauri uliotolewa na mwanasheria wa chama kwa kuwa walikuwa wameshatangazwa na vyeti wanavyo kwa mujibu wa sheria, ushindi wa ile kesi ulikuwa upo wazi, lakini yeye alizuia kesi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisisitiza kesi hiyo hata kama wangeshindwa ilikuwa na uwezo wa kukatiwa rufaa kupitia Mahakama ya Rufani  na chama kingepata haki yake ya wawakilishi wasiopungua 27 ambao wangeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

“Zanzibar hata tungeingia katika uchaguzi wa marudio, lakini tungekuwa na wawakilishi na kuwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini kwa kukaidi maagizo hayo Katibu Mkuu alitukosesha majimbo,” alisema Lipumba.

Mbali na tuhuma hizo, Lipumba pia alisema Baraza limeiagiza kamati kumuhoji Maalim Seif kuhusu msimamo wake juu ya muundo wa Muungano alioutoa kwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulienda kinyume na msimamo wa chama.

“Baraza Kuu pia limeiagiza kamati wamuhoji kuhusu msimamo wake aliyoutoa wa kutaka Muungano wa Mkataba katika Tume ya Jaji Warioba (aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya) wakati msimamo wa chama ni Serikali tatu iliyokuwa ikiungwa mkono na Tume ya Jaji Francis Nyalali.

“Alikutana na Tume akasema anataka Muungano wa Mkataba kutaka kila nchi iwe na Serikali kamili, maana yake nini? Wakati yeye ni Katibu Mkuu halafu anasema kuwa ni maoni yake binafsi, kiongozi  inakuwaje anaenda kinyume na maelekezo ya chama wakati si msemaji mkuu wa chama, hili sio jambo la kisiasa wala sio kuombea kura hiki ni kitu muhimu,” alisema.

Profesa Lipumba alisema mbali na hayo, kiongozi huyo pia amekuwa akifanya kazi za chama bila kumshirikisha Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya badala yake amekuwa akimtumia Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mazrui kinyume na Katiba ya CUF inavyoelekeza.

“Wanachama walimkubali na kwa kumuheshimu Maalim Seif  na tulipokuwa tukifuatisha ushauri wake alidhani amekuwa sultani wa chama hiki, tunahitaji nidhamu, wakati wowote akijirekebisha ofisi yake ipo.

“Msimamo wangu kama mwenyekiti ndio msimamo wa chama, wale wote watakaokiri  makosa yao na kujirekebisha kupitia kamati tunawahitaji kurudi kwenye chama, watakaoshindwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Profesa Lipumba.

Mbali na Maalim Seif, kiongozi mwingine atakayehojiwa na kamati hiyo ametajwa kuwa ni Nassor Mazrui kwa kutoa kauli za kejeli na dharau dhidi ya Mwenyekiti wa Taifa na Naibu Katibu Mkuu Bara na kuitisha vikao kinyume na Katiba ya CUF.

Alisema mbali na viongozi hao, kundi jingine litakalochunguzwa na kuhojiwa, ni wabunge na madiwani wanaodaiwa kukihujumu chama hicho.

“Wabunge ndani ya Bunge wamekuwa wakitoa matamko ya kukidhalilisha chama na kumtukana Mwenyekiti na Naibu Katibu Mkuu, kumnyanyasa mbunge wa Mtwara Mjini, Nafutaha Nachuma, kufanya hujuma katika uchaguzi wa madiwani, kumchukua mgombea na kumpeleka Chadema akagombee kwa tiketi ya Chadema Muleba.

“Kama kuna watu wataomba msamaha tutawarudisha, hatuhitaji kufukuza watu, lakini ikiwa watakaidi basi Baraza halitasita kuwachukulia hatua, hatutaki kufukuzana chama, wahojiwe wapate nafasi ya kujitetea na wapatiwe maelezo ya makosa yao kwa maandishi,” alisema Profesa Lipumba.

Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni Mazrui anayeingia kwa  cheo chake cha Naibu Katibu Mkuu, Khalifa Suleiman  ambaye ni Katibu, Masoud Muhina, Magdalena Sakaya, Hamisi Hassan, Mashaka Ngole  na Rukia Ahmed.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles