Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
MFANYABIASHARA maarufu, Yusuf Manji, amemwangukia Rais Dk. John Magufuli kwa kumwomba radhi kutokana na mvutano wake na Serikali kuhusu umiliki wa ufukwe wa Coco uliopo Bahari ya Hindi kuanzia Mnara wa Taa (Light House) hadi Bwalo la Maofisa wa Polisi (Police Officers Mess) katika Barabara ya Toure Drive, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa tangazo lililochapishwa jana katika moja ya magazeti yanayotoka kila siku (si MTANZANIA Jumapili), Manji kwa niaba ya Kampuni ya Quality Group Limited amesema kwa kutambua maelekezo ya Serikali ya Rais Magufuli, wanatii agizo lake na kuacha eneo hilo liendelee kwa matumizi kama linavyotumika sasa.
Pia tangazo hilo lilieleza kuwa Manispaa ya Kinondoni ilitangaza zabuni kupitia tangazo lake la zabuni kwa umma lililotolewa Septemba, 2005.
Tangazo hilo la Manji lilifafanua zaidi kwamba Manispaa ya Kinondoni iliagiza ombi la mapendekezo kulingana na Mfumo wa Utafiti wa Mazingira ya Jamii kuendeleza eneo la burudani lililotelekezwa kwa muda mrefu.
Kwamba masharti yaliyokuwamo ni asilimia 85 ya eneo litakaloendelezwa liwe na sehemu za wazi zenye mandhari nzuri na uwepo uwezekano wa ufukwe huo kufikika kwa urahisi kwa kuzingatia maelekezo ya mazingira ya kitaifa.
Kwa mujibu wa Manji, pia tangazo hilo la manispaa lilisema wachuuzi waliopo wasihamishwe ila wawekwe katika eneo kama ilivyowekwa katika ombi la mapendekezo jambo lililosababisha kampuni za Quality Group kushiriki katika zabuni hiyo, ikiwa ni fursa ya uwekezaji na kukuza ustawi wa jamii.
Kupitia tangazo lake, Manji alisema kwa mantiki hiyo, Quality Group kupitia kampuni yake tanzu ya Q-Consult na ikitumia wataalamu wenye uzoefu katika kuendeleza maeneo kama hayo, ilishiriki zabuni hiyo na kushinda.
Kwamba Desemba 21, 2007 pande zote mbili ziliingia makubaliano ya ukodishwaji na uendelezaji wa eneo hilo.
“Hata hivyo, kulikuwa na ucheleweshwaji kutoka Manispaa ya Kinondoni katika utekelezaji wa mradi huo, hali iliyosababisha kampuni yetu kutafuta njia za kisheria katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi mnamo Desemba 17, 2009 na kufungua kesi ya ardhi namba 334 ya mwaka 2009.
“Baada ya miaka sita kupita, Mahakama Kuu iliiagiza Manispaa ya Kinondoni kutekeleza ahadi za upande wake ndani ya wakati ili kuepuka ucheleweshwaji wa utekelezaji wa mradi,” ilisema sehemu ya tangazo hilo la Manji.
Pia lilieleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli ilipoingia madarakani ilitangaza kusudio lale la kufanya eneo hilo kubaki kwa matumizi ya wananchi kama linavyotumika kwa sasa.
Kwamba kutokana na maelekezo ya Rais Magufuli, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikata rufaa ya agizo dhidi ya Manispaa ya Kinondoni.
“Kwa kutambua maelekezo ya Serikali ya Rais Magufuli, tunatii agizo na kuacha eneo hili liendelelee kwa matumizi kama ambavyo linatumika kwa sasa,” ilisema sehemu ya tangazo hilo na kuongeza:
“Hivyo basi, tungependa kuutaarifu umma kwamba ninaomba radhi binafsi kwa Rais Dk. Magufuli na Serikali yake kwa sintofahamu yoyote iliyojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa jambo hili.
“Pia tunaomba radhi kwa usumbufu wa aina yoyote uliojitokeza kwa wadau wote tuliowakwaza wakati wa mgongano wa kisheria kwa zaidi ya mwaka mmoja jambo ambalo halikutegemewa na tunasikitika kwa hilo.
“Tumewaagiza mawakili wetu kuwa tunajitoa kama wapinzani katika rufaa iliyowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hatutadai gharama zozote zilizoingiwa au hasara ya mapato tuliyopata kwa vile masilahi yetu ya kifedha ni pungufu na si halali ukilinganisha na manufaa ya jamii.
“Mwisho, Quality Group Limited inatambua na kuunga mkono juhudi zote za Rais Dk. Magufuli za kizalendo katika kusimamia rasilimali za nchi yetu.”
Desemba 3, mwaka juzi wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi, Rais Magufuli alionya vikali juu ya njama za mfanyabiashara mmoja alizoziita kuwa zinalenga kupora sehemu ya wazi ya umma ya ufukwe wa Bahari ya Hindi inayotumiwa na wananchi wa hali ya chini kupumzika na kuogelea.