Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
MWANASHERIA nguli wa Kenya, Profesa Patrick Lumumba, amempongeza Rais Dk. John Magufuli na kusema kuwa ni kiongozi wa mfano Afrika.
Amesema kwamba kutokana na juhudi anazozifanya, katika miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa na nafasi nzuri kiuchumi, lakini akamtahadharisha asilewe sifa.
Profesa Lumumba alikuwa akizungumza jana wakati wa kongamano la tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Najua baadhi ya Watanzania wanaweza kudhani nina ajenda fulani, mimi si mwana CCM ila kuna msemo unasema mgema akisifiwa tembo hulitia maji. Kwa hiyo, naamini Magufuli atabaki kwenye njia kuu na hatachepuka, Mungu amlinde Magufuli,” alisema Profesa Lumumba.
Alisema lazima mafisadi watachukia jinsi anavyoendesha Serikali yake, lakini akamtaka asife moyo kwani kwa anayoyafanya hawezi kupendwa na watu wote.
“Kumbukeni mafisadi ni watu wa ajabu, mtu mmoja ana nyumba 40, magari 20 na mwingine unakuta anamaliza mwaka hajatembelea baadhi ya magari yake, huo ni ujinga tu, ni ulafi, ni unguruwe huo.
“Tunataka viongozi watakaoboresha miundombinu, kilimo, maisha ya wanawake na watoto. Mwafrika anataka chakula kizuri, shule, hospitali nzuri na ajira kwa vijana,” alisema.
Kuhusu sakata la mchanga wa madini, Profesa Lumumba alisema Rais Magufuli yuko sahihi kwa anachokifanya.
“Nilisoma magazeti ya Tanzania, kwamba bosi wa Acacia alikwenda Ikulu akasema nimekosa sana na Rais Magafuli akamwambia nimekusikia mwanangu, tutakuhurumia, lakini kwa masharti na lazima ulipe fedha ulizopora,” alisema Profesa Lumumba.
Pamoja na hayo, aliwatahadharisha viongozi kuacha kujiona miungu watu kwani hali hiyo inachangia mdororo wa kisiasa na kiuchumi.
“Unakuta kiongozi analindwa na askari zaidi ya 50, sasa kama ulichaguliwa kihalali na wananchi, kwa nini unawaogopa?”alihoji.
Wakati huo huo, Profesa Lumumba aliwachambua baadhi ya viongozi wa Afrika kwa kueleza udhaifu wao na wema walioufanya.
Baadhi ya viongozi hao ni Hayati Idi Amin (Rais wa Kwanza wa Uganda), Robert Mugabe (Rais wa Zimbabwe), Dk. Kenneth Kaunda (Rais wa Kwanza wa Zambia), Muhammadu Buhari (Rais wa Nigeria) na Paul Kagame wa Rwanda.