Pyongyang, Korea Kaskazini
ALIYEKUWA nyota wa mpira wa kikapu Marekani, Dennis Rodman amefanya tena ziara nchini Korea Kaskazini ambayo ina mgogoro mkubwa na Marekani.
Nyota huyo wa zamani wa NBA anafanya ziara ya binafsi kwa mara ya tatu.
“Ninajaribu tu kufungua mlango, nina furaha kuwa Rais Trump anafurahia kwa sababu mimi niko hapa na ninajaribu kutimiza kitu fulani ambacho sisi sote tunahitaji,” alisema Rodman.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Beijing akielekea Korea Kaskazini.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Rodman anafanya ziara ya urafiki na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un. Awali alitembelea nchi hiyo mwaka 2013 na 2014.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema inafahamu ziara yake.
“Tunamtakia mema lakini tumetoa onyo kwa raia wa Marekani na kuwashauri wasisafiri kuenda nchini humo kwa usalama wao,” alisema Naibu Waziri wa Mambo ya Mje wa Marekani, Thomas Shannon.
Mgogoro kati ya Marekani na Korea Kaskazini umekuwa mkubwa wakati huu wa utawala wa Rais Donald Trump, ambaye anasema anahofia mzozo mkubwa huenda ukaibuka kati ya nchi hizo mbili.
Rais Trump pia amesema kuwa angependa kukutana na Rais Kim wa Korea Kaskazini.