32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MZEE NGOSHA HAKUSTAHILI KUFA KWENYE DIMBWI LA UMASKINI

NA CHRISTOPHER MSEKENA

MAPEMA wiki hii sekta ya sanaa ilipata pigo la kuondokewa na msanii wake mkongwe katika uchoraji, Francis Maige Kanyasu, maarufu kama Mzee Ngosha, ambaye inadaiwa kuwa ndiye mbunifu na mchoraji wa Nembo ya Taifa (Bibi na Bwana).

Msiba huu umewagusa Watanzania wengi ambao asilimia kubwa walianza kumfahamu baada ya kuonekana kwenye taarifa ya habari ya kituo fulani cha runinga akiwa kwenye mazingira ya dhiki yaliyochangia afya yake kudhoofu.

Moja ya wasanii walioguswa na kushtushwa na kifo cha Mzee Ngosha, ni Mrisho Mpoto ambaye anadai kuwa mzee huyo aliwahi kuibuka ‘location’ wakati wa utengenezaji wa video ya wimbo wake wa Njoo Uchukue, alitoa maelekezo mazuri ya kuipendezesha video ile huku akitaka ashiriki kama Mzee Mshuba, kikongwe muuza bangi aliyeimbwa ndani yake.

Hiyo ni ishara tosha kuwa Mzee Ngosha ni msanii wa siku nyingi, mbunifu aliyefanya sanaa yenye thamani kubwa lakini ameishia kupoteza maisha akiwa kwenye dimbwi la umasikini.

Kifo cha Mzee Ngosha pia kimemgusa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye alitoa ubani na salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki, huku akimwelekeza Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa, Godfrey Mngereza, kushirikiana na ndugu katika shughuli zote za mazishi.

Lakini pia Waziri akaahidi michango ya wasanii wakongwe kwa Mzee Ngosha inalindwa kwa ajili ya faida ya kizazi kijacho. Inaweza kuwa ni dalili nzuri kwa wasanii hasa wanaofanya sanaa hizi za uchoraji kupata nafasi ya kuthaminiwa zaidi.

Mzee Ngosha aliubeba utajiri ndani ya kipaji chake, lakini kutokana na kutokuwa na miundombinu rafiki kwa wasanii wa sanaa hiyo, hakuna aliyejua uzito wa utajiri wake kiasi kwamba yeye mwenyewe akaona ni kawaida kuishi maisha yale.

Kumekuwa na sintofahamu nyingi kuhusu ukweli wa aliyechora Nembo ya Taifa, maana baada ya Mzee Ngosha kutangaza kuwa alibuni na kuchora nembo hiyo, kuna familia ilijitokeza ikidai kuwa mzee wao ndiye aliyechora.

Tuachane na habari hizo ambazo zinahitaji utafiti na uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli. Tubaki kwenye lengo la kuifanya sanaa izalishe matajiri, ili hata watakapotoweka kwenye uso wa dunia tutambue sanaa iliwanufaisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles