UCHAGUZI KENYA KUKWAMISHA KIKAO CHA BUNGE EALA

0
952

Na JANETH MUSHI,

ARUSHA

BUNGE la 4 la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), linalotarajia kuanza Juni 5 mwaka huu, linaweza kukwama kuanza kutokana na uchaguzi wa wabunge kutoka Kenya kuchelewa kufanyika.

Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Arusha na Spika wa Bunge hilo, Daniel Kidega, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa Bunge la 3 la Jumuiya hiyo.

 Spika huyo alisema kuwa, mpaka sasa ni nchi tano tu ambazo ni Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani ya Kusini zimeshafanya uchaguzi wa wabunge wake watakaowakilisha nchi zao katika Bunge hilo.

Alisema Kenya pekee ndiyo haijafanya uchaguzi wa wawakilishi wake mpaka sasa, jambo linaloweza kuchangia kukwama kuanza kwa Bunge hilo, kwani lazima wawakilishi wa nchi zote wawepo ndipo bunge lianze.

Kidega alisema watawasiliana na Serikali ya Kenya, likiwamo Bunge ili uchaguzi huo ufanyike haraka na kuwa hawataki vikao vichelewe kuanza kama ilivyokuwa mwaka 2006 ambapo vikao vya bunge hilo la pili vilichelewa kuanza kwa miezi 6 kutokana na kuchelewa kwa uchaguzi wa wabunge.

"Kuna changamoto kutoka Kenya, nchi nyingine wameshamaliza kufanya uchaguzi wa wabunge wa Bunge la 4, tunaomba Kenya iharakishe kufanya uchaguzi wa wawakilishi wao, hatutaki tatizo kama lililotokea bunge la pili ambalo lilichelewa kuanza kwa miezi sita na tatizo la Kenya ni uchaguzi wa wabunge wa EALA kuingiliana na uchaguzi mkuu," alisema.

"Aidha, tunawashukuru sana waandishi wa habari namna mlivyotusaidia kufanya kazi zetu kama Bunge, tumeshirikiana kwa pamoja na sasa wananchi wengi wa nchi wanachama wanajua nini kilikuwa kinafanyika. Nawashukuru pia viongozi wa nchi zote za Jumuiya wamesaidia kwa kiasi kikubwa bunge hili la tatu," aliongeza  Spika huyo.

Aidha, katika kikao hicho cha mwisho, Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Shyrose Bhanji, aliwasilisha hoja binafsi iliyoungwa mkono na wabunge wengine, kuhusu maazimio ya kuwapo mtaala wa pamoja wa elimu katika Shule za Msingi na Sekondari za nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here