NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
WAKULIMA wadogo nchini Tanzania wapo mbioni kupata taarifa mbalimbali za kidijitali kuhusu masuala ya pembejeo, ukiwamo ushauri utakaosaidia kutatua matatizo yanayowakabili kama vile upatikanaji wa fedha, pembejeo na mafunzo.
Mradi huo umezinduliwa jana na taasisi tatu za Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA), Positive International Limited (PIL) na Grameen Foundation katika sherehe zilizohudhuriwa na maofisa wa Serikali, wawakilishi wa vyama vya wakulima, taasisi za fedha, kampuni za mbegu, wafanyabiashara wa nyenzo za kilimo na wale wanaojishughulisha na biashara za mazao ya sekta ya kilimo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Positive International, Karan Kapoor, alisema Dar es Salaam jana kuwa matumizi ya dijitali kwa mauzo ya pembejeo za kilimo nchini Tanzania ni makubwa.
Alisema wakulima wanaotaka kuwekeza katika kilimo cha kisasa wanashindwa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha kwa vile ni asilimia 6 tu ya mikopo ya benki ndio imetengwa kusaidia sekta ya kilimo.
Kapoor alisema wakulima wanatumia fedha zao chache kununua pembejeo za kilimo kutoka kwa walanguzi, pembejeo ambazo mara nyingi hazina uthibitisho wa ubora.
“Kifaa hicho cha digitali kitawawezesha wakulima kulipia mapema pembejeo wanazohitaji kupitia simu za mkononi kwa bei nafuu. Pia kitawapa wakulima pembejeo kulingana na mazao na malengo yao ya uzalishaji na pia kupata taarifa za ushauri kuhusu matumizi bora ya pembejeo hizo,” alisema Kapoor.
Naye kiongozi anayeshughulikia masuala ya fedha wa Shirika la Alliance For Green Revolution Afrika (AGRA), Headwing Siewertsen, alisema moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wakulima ni ukosefu wa fedha mwanzoni mwa msimu wa upandaji mazao, jambo ambalo huwalazimisha kutafuta fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo na hivyo kuwaongezea mzigo.
“Kifaa hicho cha dijitali kwa ajili kusaidia upatikanaji pembejeo za kilimo ni ufumbuzi wa kipekee kwani kitawaimarisha na kuwasaidia wakulima kutenga fedha kwenye akaunti zao za simu ili waweze kununua pembejeo bora kwa muda mwafaka na kwa bei nafuu ya asilimia 30,” alisema Siewertsen.
Alisema wakulima wadogo nchini Tanzania huzalisha asimia 70 ya chakula ingawa karibu nusu yao hawazalishi chakula cha kutosha kwa ajili ya mauzo.
Siewertsen aliongeza kuwa wakulima wa Tanzania wanakabiliwa na ukosefu wa teknolojia ya kilimo cha kisasa, hawana uwezo wa kujipatia pembejeo bora na wanakosa huduma za kiufundi za ugani zinazoweza kuwasaidia kukuza kilimo pamoja na ukosefu wa mafunzo.
“Wakulima hawa wanategemea zaidi kilimo cha mvua, zana duni za kilimo na mbegu hafifu ambazo ubora wake hupungua kila msimu wa kilimo,” alisema Siewertsen.