33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KWAHERI MWALIMU CHRIS, ULIKUWA MWANGA YETU

NA SARAH MOSSI


KIFO ee kifo, kifo hakina huruma! Ilikuwa ni Jumapili takribani saa 1:56 asubuhi nikijiandaa kuamka. Nina kawaida ya kuangalia simu yangu kuona ni meseji gani zimeingia katika simu yangu nikiwa nimelala na kuzipitia ili nianze siku.

Mara nyingi nilizoea kukutana na meseji za rafiki zangu, ndugu yangu Masyaga Matinyi ambazo kimsingi meseji zake nyingi zilikuwa zikinifurahisha usiku kucha akinitania huku akijua kwa namna moja au nyingine baadhi ya meseji zake zilikuwa zikitaka kuamsha hasira kwa makusudi lakini kwa vile nimemzoea, najikuta nikizifurahia.

Hafla! Lahaua inaingia meseji ya GME, Absalom Norman Kibanda ikisomeka hivi: MSIBA: Kwa maandishi makubwa! Lahaula nikajikuta naruka kitandani kufukuzia miwani yangu maana bila ya kuvaa miwani siwezi kusoma vizuri. Na baada ya kuvaa miwani nikaendelea kusoma andiko la Absalom:

MSIBA:

Kwa masikitiko makubwa. Ninachukua fursa hii kwa uchungu mkubwa kuwatangazia wafanyakazi wa NHL kwamba Kaka yetu na mzee wetu, Mwalimu Chrisostom Rweyemamu amefariki dunia usiku wa kuamkia leo wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.

GME.

Kabala hata sikumalizia kuisoma meseji hii nilijikuta nikipiga yowe kubwa sana lililowaamsha baadhi ya ndugu zangu na kuuliza kulikoni, nikawapa simu wasome meseji, waliposoma nao walianza kuuliza huyu ni nani, nikawaeleza huku nikiomboleza, Na kwa kweli kuanzia hapo sikujitambua kwa maana akili yangu ilikuwa haijui inafanya kitu gani zaidi ya kuomboleza Mwalimu wetu.

Nilivyomfamhamu Mwalimu

Zaidi ya miaka kumi sasa nimefanya kazi katika kampuni hii ya NH (2006) Ltd wakati huo nilipojiunga nayo ilikuwa ikiitwa New Habari  Ltd, kati ya watu niliokuwa nikiona wako makini na kazi yao basi ni Mwalimu Chriss kama wengi walivyozoea kumwita.

Enzi za uhai wake Mwalimu alikuwa msimamizi mkubwa wa wafanyakazi na anapoona mfanyakazi amekaa akizurura au akifanya maongezi huku akiacha kufanya kazi yake alikuwa na staili fulani ya kumuangalia huyo mfanyakazi, mara nyingi alikuwa hakusemeshi lakini alikuwa na jicho fulani akikuangalia unaanza kujua hapo ni lazima umefanya kitu kinakwenda kinyume na maadili ya kazi yaliyokupeleka NHL.

Mwalimu aliendelea kuwa msimamizi mzuri wa wafanyakazi na hata ikitokea mmekwaruzana naye, basi huwezi kumsikia Mwalimu akipayuka badala yake utamuona Mwalimu akiinamisha kichwa chake na kunyoosha kidole huku akisisitiza jambo lake.

Kwangu mimi hali hiyo ilijenga heshima kubwa kwa Mwalimu na pengine katika kipindi chote nilichokuwa hapa nilijenga heshima kubwa kwa Mwalimu lakini sikuacha tabia yangu ya kumtania pale ninapomuona Mwalimu pengine siridhishwi na majibu yake.

Nakumbuka katika kikao kimoja cha Post morterm ambacho Mwalimu alikuwa ndio msimamizi Mkuu hadi anafariki, ambacho alihudhuria GME, Absalom alituletea baadhi ya wafanyakazi ujumbe fulani (ambao kiukweli naamini ujumbe huo haukuwaridhisha wafanyakazi waliousikia), baada ya kumsikiliza kwa makini, akamalizia na maneno “Nimeleta ujumbe huu na mjumbe hauawi”

Kukatokea kimya cha sekunde kadhaa, lakini mimi kwa ujasiri bila ya ridhaa yake nikamjibu “ Mwalimu iko siku mjumbe atauawa” Hakika maneno haya yalimfurahisha kila aliyeisikia kauli hiyo akiwamo Mwalimu mwenyewe. Na kikao cha Postmortem kikaishia hapo.

Baada ya hapo Mwalimu alinifuata akanieleza hivi “ Wewe ni matata sana” nikamjibu “ Mwalimu siku nyingine usikubali kuleta ujumbe hasa unaohusiana na masilahi ya wafanyakazi” akacheka sana huku akitikisha kichwa.

Kuanzia siku hiyo nikajenga utamaduni wa kumtania Mwalimu kila ninapomuona lakini utani wangu sio ule wa kumvunjia heshima na ikitokea hakuniona siku kadhaa kazini huniuliza “Ulikuwa wapi Sarah”

Kuumwa kwake

Kuumwa kwa Mwalimu ni kama vile kulikuja ghafla kwani mara nyingi tulizoea kumuona Mwalimu akiwa smart mwenye afya nje lakini mara baada ya kwenda safari yake ya matibabu nchini India, aliporudi, nilimuona Mwalimu ni kama vile amebadilika tabia yake.

Mwalimu alikuwa mpole sana sio yule niliyezoea kumuona na wakati fulani akiwa kwenye ofisi yake nilimuona Mwalimu akiwa pekee na mnyonge sana. Hali hii iliniumiza sana na nakumbuka siku moja nilimfuata ofisini kwake nikamuuliza Mwalimu kwanini unakuwa mnyonge sana, hakunijibu, alitabasamu tu.

Nikamwambia Mwalimu najua unaumwa lakini ukiwa mnyonge kiasi hiki unazidi kujiongezea maradhi, ni lazima uchangamke kama vile nilivyozoea kukuona. Akanijibu sawa hili lisikupe tabu.

Kitaaluma

Wengi wamemwelezea Mwalimu juu ya umahiri wake katika taaluma na mimi nikiyaandika hapa ni kama vile nitakuwa nayarudia tu. Lakini Mwalimu alinisaidia sana katika kuboresha kazi zangu katika Jarida la Siasa. Na wakati mwingine sikuacha kumpinga pale ninapoona kile anachonieleza sikubaliani nacho. Lakini kwa upole Mwalimu alinirejesha kwenye mstari na kwa umahiri mkubwa nakubaliana naye.

Mwalimu alikuwa ni mzazi kwetu, nakumbuka mara fulani tunamkosea na Mwalimu ukimkosea haoneshi hasira badala yake kwa upole atakuangalia na kuinama chini. Niseme wazi sikuwahi kumuona Mwalimu akikasirika na kutoa kauli za vitisho vya kuogopesha.

Mwalimu alikuwa ni mtu wa pekee kwetu, hata ukionesha kumpinga haonekani kukasirika badala yake utamuona akizungumza na wewe kwa upole na kwa kutumia mbinu zake za kiualimu atahakikisha unakubalina naye.

Umuhimu wa mwanadamu huonekana pale anapokuwa ameondoka au anapoiaga dunia na hiki ndicho ninachokiona kwa Mwalimu. Mwalimu ameondoka na tunafikiria wakati atakapokuwa hayupo kabisa nani atavaa viatu vyake.

Mwalimu Kwaheri, Mwalimu umeondoka bila hata kutupa neno la Mwiso

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles