25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

PEMBEJEO FEKI ZAWALIZA WAKULIMA

NA GORDON KALULUNGA-MBEYA


WAKULIMA wa zao la Kahawa Wilaya ya Mbeya, wamelalamikia uzagaaji wa pembejeo feki katika maduka mbalimbali wilayani humo zinazoathiri mazao yao.

 

Hayo waliyasema jana katika mkutano mkuu wa Chama cha Ushirika Usongwe (AMCOS )uliofanyika katika ofisi za chama hicho zilizopo Kijiji cha Iwindi wilayani humo.

 

Akichangia hoja katika mkutano huo, mkulima Julius Mzumbwe, alisema inashangaza kuona uongozi wa chama unawauzia pembejeo kwa ongezeko la Sh 500 tofauti na gharama wanayouza katika maduka ya watu binafsi.

 

Akijibu hoja hiyo, Katibu Msaidizi wa ushirika huo, Godfrey Mwakalonge, alisema hali hiyo inatokana na uendeshaji, pia pembejeo

wanazowapatia zinakuwa hazina shaka katika ubora wake.

 

“Ndugu zangu wajumbe, mbali na gharama za usafiri, upakiaji, upakuaji na ugawaji, lakini tunazingatia ubora wa pembejeo tofauti na kuzinunua kwenye maduka kama mnavyokumbuka tumewahi kununua pembejeo kwa akina Kalinga Agro yaliyotukuta sote ni mashahidi kumbe Coper walituuzia Matofali,” alisema Mwakalonge.

 

Akikazia majibu hayo, Mwenyekiti wa bodi ya ushirika huo, Jailos Mwashigala, alisema mbali na pembejeo nyingi madukani kuwa feki, pia wafanyabiashara wanapunguza ujazo kwa kila pembejeo zikiwemo mbegu na dawa mbalimbali.

 

“Mkitaka kujua zaidi waulizeni wakulima wa vijiji vya Shongo na Holongo, Kata ya Igale hao wanajua zaidi athari za kununua pembejeo

katika baadhi ya maduka ya pembejeo hasa yaliyopo Mbalizi,” alisema.

 

Mbunge wa kwanza wa Jimbo la Mbeya aliyetawala kwa miaka 15, ambaye pia ni mwasisi wa chama hicho cha ushirika mwaka 1968, Patrick Nswilla ambaye alihudhuria pia mkutano huo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa pembejeo feki zinazidi kushamiri wilayani humo kutokana na vitendo vya rushwa.

 

“Tangu muda mrefu wakulima wanalalamika maana wafanyabiashara huwa wanasaga matofali ya kuchomwa na kuyaweka kwenye mifuko wakiuza kama Copper, huku unga huo wa matofali wakipaka mahindi na kuziuza kama mbegu bora,” alisema Nswilla.

 

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Oran Manase Njeza, alipoulizwa kama anafahamu kadhia hiyo, alisema kosa hilo ni la jinai na amewataka wakulima ambao wanapata matatizo hayo wayapeleke Polisi ili hatua zichukuliwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles