25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA YAIPIGA MBAO FC 2-1, WABEBA KOMBE LA SHIRIKISHO

 

 

SAADA SALIM NA ZAITUNI KIBWANA, DODOMA

KLABU ya Simba SC, imefanikiwa kurudi katika michuano ya kimataifa baada ya miaka mitano, kufuatia jana kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA CUP), kwa kuifunga Mbao FC 2-1 Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Mara ya mwisho, Simba kushiriki michuano ya kimataifa ilikuwa mwaka 2013 baada ya  kufungwa na CR Libolo ya Angola kwa mabao 4-0 kwenye mchezo wa Klabu Bingwa Afrika. Kabla ya hapo Simba ilipoteza, mbele ya Al Ahly Shandy ya Sudan kwa mikwaju ya penalti 3-1 mwaka 2012.  

Haikuwa kazi rahisi kwa Simba kupata nafasi ya kupanda ndege kwani ililazimika kucheza dakika 120 baada ya kumaliza dakika 90 wakiwa sare ya bao 1-1.

Simba walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 95 katika kipindi cha kwanza muda wsa nyongeza kupitia kwa mshambuliaji wake Fredrick Blagnon aliyepokea pasi kutoka kwa Abdi Banda na kuachia shuti kali kwa guu lake la kushoto lililoingia moja kwa moja nyavuni.

Lakini mambo yalibadilika tena uwanja wa Jamhuri baada ya Mbao FC kusawazisha dakika ya 104 kupitia kwa mchezaji wake Ndaki Robert ambaye alitokea benchi.

Simba wakamaliza mchezo huo dakika ya 120 baada ya Shiza Ramadhani Kichuya kuwainua mashabiki wao kwa mkwaju wa penati baada ya beki wa Mbao kushika shuti la beki Murshid Juuko lililokuwa linaingia moja kwa moja nyavuni na mwamuzi Ahmed Kikumbo kuamua penati.

Katikia dakika 45 za kwanza, mshambuliaji Laudit Mavugo kama angekuwa makini angeweza kuipatia timu yake mabao mengi baada ya kupata nafasi nzuri dakika 4, 9, 12, 22, 26, 33 na 34 lakini alishindwa kufanya hivyo.

Mbao walianza vizuri ambapo dakika ya nne walifika langoni mwa Simba baada ya kipa wa Simba, Daniel Agyei kutema vibaya mpira wa faulo uliopigwa na Salmin Hozza na kutua miguu mwa Pius Buswita lakini alipiga pembeni.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kila timu ikiwa ikitaka kumaliza mchezo dakika 90, lakini milango ya timu zote ilikuwa migumu.

Beki wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alitolewa nje kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuugulia maumivu, mchezaji huyo tangu msimu uanze amekuwa akicheza dakika zote.

Katika mchezo huo Simba waliingia na aina ya kipekee, baada ya kuingia uwanjani na wachezaji wote kuinama kwenye viatu vyao na kufunga kamba wakiashiria wapo tayari katika vita.

Kabla ya mchezo kuanza Kichuya pamoja na Vincent Costa na Mosses Kitandu waliingia uwanja na kuwasalimia mashabiki na kisha kurudi ndani.

Mbao FC nao kipindi cha pili waliingia na kujipanga golini huku wakiwa wamepiga magoti kwa mstari na kuomba dua.

Mashabiki walianza kuingia asubuhi kwa ajili ya kuwahi nafasi na mpaka saa tano uwanja ulikuwa umejaa kila sehemu.

Katika hatua nyingine, Bodi ya Ligi Kii Bara imemtangaza mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa, kuwa mfungaji bora wa michuano ya Kombe la FA baada ya kufunga mabao matano huku James Kotei akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa fainali.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles