24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

NCHI IMEGEUZWA KUWA KISIWA CHA ‘WAKWEPA KODI’

 

 

NA MARKUS MPANGALA,

JOGOO awike au asiwike, wanasema hawana faida wanayopata katika uchimbaji wa madini. Usiku uje na uondoke, mchana uje na uondoke, bado habari inakuwa ileile, wawekezaji au tuseme kampuni za uchimbaji wa madini zinalalama hakuna faida wanayopata kwenye migodi yetu ya madini.

Mvua inyeshe au isinyeshe, jua liwake au lisiwake, bado habari ni ileile kwamba hakuna faida kwenye madini yetu. Habari hii imechukuliwa kwa zaidi ya miaka 17 sasa na simulizi zimekuwa zilezile, hakuna faida.

Mabadiliko ya majina ya kampuni, yanakuja na kuondoka. Mabadiliko ya wamiliki wa migodi ya dhahabu wanakuja na kuondoka. Habari ni ileile hakuna faida. Sasa kama hakuna faida viweje waendelee kuchimba madini kwenye migodi yetu?

Ukigeukia ughaibuni kwa wataalamu wa masuala ya biashara na uchumi, wanapozungumza au kuonyeshwa kwenye televisheni kama za Bloomberg TV na nyingine utaona majina ya kampuni zilezile zikitajwa kuvuna faida.

Ripoti mbalimbali za kibiashara na uchumi kama LHRC utaona zinashangaa inakuwaje fedha zinayeyuka kama moshi wa angani huku mamlaka zinazohusika zipo. Utaona ripoti zinasema kuwa kampuni Fulani ya madini nchini Tanzania imepata faida kiasi Fulani kwa kipindi cha nusu mwaka ua mwaka mzima.

Kampuni hizo hizo kwenye miji yenye masoko makubwa ya hisa kama ya London (Uingereza), Tokyo (Japan), Beijing (China), New York au mitaa ya vibopa  kama Wall Street wasemako fedha hailali (Money Never Sleep) huko Marekani habari inakuwa ileile, kampuni inakuwa ileile, majigambo yaleyale ya kuvuna faida kubwa.

Hapa kwetu tunaambiwa habari ni mbaya kwamba hakuna madini hayazalishi faida. Lakini kule ughaibuni tunaambiwa faida ni kubwa mno na wanaalikana kuja kuwekeza kwa kutumia ununuzi wa kubadilisha majina ya kampuni.

Swali linabaki pale; viweje kama kuna hasara ya uchimbaji wa madini bado wahusika wakaendelea kunufaishwa na misamaha ya kodi?

Pamoja na makosa yetu kwenye mikataba ya sekta ya madini, huwa ninajiuliza swali hili; ni kwanini kampuni au wawekezaji katika uchimbaji wa madini kwenye migodi yetu wakati wote wanalalamika kutopata faida katika shughuli zao? Kwamba tangu zianze kazi hazijawahi kusema zimepata faida, ni kwanini?

Swali hilo limekuwa likizingira akili yangu na wakati mwingine ninabaki na masikitiko juu ya hatima ya nchi hii katika sekta ya madini.

Mosi, rafiki yangu mmoja ameniambia jibu rahisi la swali langu ni kwa sababu Sheria ya Madini ya mwaka 1998 imewapa nafasi ya kufanya hivyo. Ameniambia kuwa, hata yeye mshahara wake unakatwa kodi kabla hata haujamfikia, haijalishi kama unabakia ama unamtosha. Anasema hata duka la Mangi mtaani anatandikwa kodi bila kujali kama ameuza ama hajauza bidhaa yoyote.

Pili, rafiki yangu mwingine amenituma kwenu Watanzania wengine, hususani watumishi wetu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) niwaulize swali moja. Yeye amenituma niseme hivi: “Naomba uwaulize TRA kuhusu kitu kinaitwa Holiday Tax (Grace period) katika uwekezaji mkubwa angali mfanyabiashara mdogo hapo kijiweni akiweka kibanda kando ya barabara wanataka aende TRA kukadiriwa tozo ya kodi hata kabla hajajua kama bidhaa atakazouza zitapata wateja wa kumpatia faida ili kufidia mtaji wake.

Ameniambia niulize tena: “Jambo lingine ni kuwa hizi nchi maskini katika teknolojia huwa zinasikiliza wenye teknolojia wanasemaje. Hivyo, angalia wanavyopeana ulaji katika muda mfupi. Kutoka kampuni moja ya madini hadi nyingine (majina yanahifadhiwa) hapa kuna tatizo la kukwepa kodi pindi wanapouza hisa kwa kampuni fulani.

Vilevile alisema: “Nitakupa mjadala mmoja ambao nadhani unaweza kuisaidia nchi yetu kidogo kama watakubali, kwani uthubutu anaoufanya JPM kwa sasa ulishafanywa na nchi za Ulaya kama Norway kwenye uwekezaji wa gesi na mafuta.”

Sasa tujadiliane. Baada ya hapo mimi na wewe msomaji tujiulize swali moja muhimu; Tumewafukuza mawaziri wangapi waliokuwa kwenye Wizara ya Nishati na Madini, lakini hakuna mabadiliko yoyote ya msingi kuhusiana na Sheria pamoja na mikataba ya sekta ya madini?

Uamuzi wetu wa kuwafukuza mawaziri tunaweza kuungana kuwa ni mzuri. Lakini hauwezi kuwa mzuri zaidi iwapo tutakuwa tunacheza sendema kila wakati. Kwamba badala ya kupiga hatua katika maendeleo yatokanayo na madini, bado tumekuwa taifa la kufukuza na kubadilisha watu pasipo hatua za msingi kuchukuliwa.

Kila awamu tunafukuza mawaziri, lakini sheria haibadiliki. Kila awamu tunaendelea kuambiwa migodi ya madini haizalishi faida, badala yake kampuni ziendelee na uchimbaji.

Ninadhani hii si busara hata kidogo, bali ni kukumbatia ufukara kwa matumaini hewa na kusaini makaratasi yanayoonyesha hakuna faida pasipo kufanya ukaguzi kwenye ‘field’.

Kutoka mwaka 2002 tumekuwa tukifukuza mawaziri wizarani. Na mwaka huu tumemfukuza waziri ambaye tuliwahi kumfukuza kwanza, je, tatizo letu ni mawaziri pekee au suala jingine la kodi na sheria za madini?

Nakuachia tafakari ndogo tu kwa leo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles