KUNA maudhi mengi kwenye uhusiano, lakini kubwa zaidi ni ile ya kupotezewa muda kisha kuachwa. Hili huwatokea zaidi wasichana.
Anakuwa na penzi la dhati kwa mwanaume, anawekeza muda na mapenzi yake ya dhati lakini mwisho wa siku, kumbe jamaa hana time naye.
Amemfanya demu wa kuzugia. Wanawake wanapenda kuwajua vizuri wanaume wanaokuwa nao, lakini wanaume ni wajanja sana na wanaweza kujificha wasigundulike kirahisi kinachoendelea kwenye uhusiano wanaokuwepo.
Kujua inasaidia kuchukua hatua. Tatizo ni kwamba wanawake wengi wakipenda, husahau kila kitu. Wao hubaki na jambo moja tu; wanapenda! Mengine hawana time nayo.
Inawezekana kuna mengi ya kufanya ili kumjua mwanaume wako, lakini hapa nimekuandalia dondoo chache.
MWEKEE MITEGO
Kitu muhimu zaidi cha kufanya ili kumjua mwanaume wako ni kumfuatilia kwa karibu. Fanya hivyo kwa kutumia ujanja wa hali ya juu ili asijue kuwa unamtega.
Atafanya mambo yake gizani mpaka lini? Kuna siku utagundua na kumuacha aendelee na umalaya wake kama ameona ndiyo maisha.
Usikubali kabisa kuwa katika penzi la kitumwa, penzi la kisaliti, kuwa na mtu ambaye anakuchanganya wa kazi gani zaidi ya kukupotezea muda na kukukaribishia machozi?
HATAKI UJULIKANE
Hii ni alama nyingine walizonazo matapeli wa mapenzi, ni watu wa kufanya mambo kwa upekee sana. Kila dakika hakaukiwi na neno nakupenda sana, lakini moyoni mwake hakuna alama hata moja ya mapenzi kwako.
Ni vigumu kumtambua mtu wa aina hii lakini chunguza kuhusu hili, hapendi kabisa kukukutanisha na rafiki zake na hata mkikutana nao kwa bahati mbaya basi hatakutambulisha na kama akikutambulisha hatakutambulisha kama mpenzi wake rasmi.
Ataishia kusema ninyi ni marafiki mlioshibana! Tangu lini mpenzi akatambulishwa kama rafiki? Baadaye utakapomuuliza hawezi kuwa na jibu la maana, atabaki kukuambia hata kama akikutambulisha kama rafiki, jamaa ataelewa kuwa ni mpenzi wake, hii inaingia akilini kweli?
Huo ni ulaghai na anaogopa kukutambulisha kama mpenzi maana tayari ameshaonwa akiwa na wapenzi wengine. Jiulize, ikiwa leo hii anashindwa kukutambulisha vyema kwa rafiki zake, vipi kwa ndugu zako?
Ataweza kuwa na ubavu wa kufika kwa wazazi wako na kufuata taratibu zote za ndoa?
MSIRI KUPITILIZA
Hii ni alama nyingine waliyonayo wanaume wa aina ninayoielezea katika mada hii. Siku zote mambo yao ni kwa siri kubwa, kama mna ahadi ya kukutana, hataki muongozane, atakuambia mkutane moja kwa moja sehemu husika.
Hata muda wa kuondoka atafanya kila njia ili kila mmoja aondoke mwenyewe na kama mkiondoka pamoja basi ujue ni usiku na hakuna atakayewaona.
Ikitokea akakubali kuongozana na wewe, hatapenda muongozane pamoja. Atalazimisha utangulie mbele yeye afuate nyuma, kwa nini? Kwa sababu anaogopa kujulikana kuwa yeye ni mpenzi wako.
Fikiria, kama anaogopa, anakupenda kweli? Mapenzi gani hayo yanafanywa kwa siri? Anakupotezea muda huyo.
HAPENDI NDUGU WAFAHAMIANE
Mpenzi wa aina hii ni mjanja sana, kwanza kabisa atajifanya mtu mwenye ubize sana, yote hii ni kukwepa kuwajua ndugu zako au wewe kuwajua ndugu zake!
Wakati mwingine anakuwa hapendi ndugu zako na wake wakutane wakijua wazi kuwa nyie mna uhusiano, hili ni tatizo.
Hakuna uhusiano wenye heri na malengo ya kuishi pamoja siku zijazo ukawa wa kificho cha kiasi hicho. Kama ana nia na wewe basi atahakikisha anawafahamu baadhi ya ndugu zako na wewe unawafahamu baadhi ya ndugu zake, hayo ndiyo mapenzi ya kweli.
Mapenzi hayaishii kwa nyie wawili pekee bali hata kwa ndugu zenu. Mnapojuana inakuwa rahisi kusaidiana hata katika mambo mengine ya kawaida.
Lakini kumbuka, jambo hilo haliwezi kuwa la muhimu, wakati mwenzako hana wazo la kukuoa! Wakati ukiwaza maisha, ukiwa na ndoto za kuolewa naye, mwenzako anawaza ngono tu.
Rafiki yangu, mwili wako una thamani kubwa sana, uheshimu. Usijishushe kiasi hicho, ukigundua hayo na mengine yanayofanana na hayo ni bora kuchukua hatua kwa kuangalia ustaraabu mwingine.
Kumbuka huyo anayekupotezea muda na kukuchezea hivi sasa, hana thamani kama aliyeandaliwa kwa ajili yako. Yupo lakini hujakutana naye – ni muda tu.
Je, unapenda kujifunza masomo haya zaidi kupitia group la WhatsApp la Love Moment? Kama ndivyo karibu inbox, andika ujumbe wako ukitaka kujiunga na kundi hilo, nasi tutakuunganisha.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, aliyeandika vitabu kama True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.