30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

MTOTO WA KADA CCM ALIYEPIGWA RISASI KIBITI AFARIKI DUNIA

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


WAKATI Jeshi la Polisi likiendelea kuimarisha ulinzi wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani, simanzi imezidi kutawala baada ya mtoto wa Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Iddy Kirungi aliyejeruhiwa kwa risasi tumboni, kufariki dunia.

Mtoto huyo, Nurdin Kirungi, alifariki dunia saa mbili usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa kwa matibabu tangu alipojeruhiwa.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Steven, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.

“Ni kweli Nurdin hatupo naye tena duniani, tangu usiku wa kuamkia jana,” alisema.

MTANZANIA lilipohoji iwapo mwili wake umeshachukuliwa kwa maziko au la, Steven alitaka watafutwe ndugu wa marehemu kwani suala hilo lipo chini ya mamlaka yao.

“Ndugu ndiyo wanaweza kueleza juu ya hilo, sisi tunathibitisha tu, kweli ametutoka,” alisema.

Akizungumza na MTANZNIA kwa simu jana, Diwani wa Kata ya Mtunda, Twanga Omary, alisema familia ya marehemu imeanza utaratibu wa maziko ya ndugu yao.

“Huku Mtunda ni kama vile tupo kisiwani, nipo shamba na kuna mvua kubwa inanyesha, mito imefurika maji, nimeshindwa kufika msibani, niliwasiliana na wanafamilia wamenijulisha wameanza utaratibu wa maziko,” alisema.

Alisema hadi jana mchana mwili wa marehemu ulikuwa haujafikishwa nyumbani.

“Bado haujafikishwa kutokana na mvua zinavyonyesha, natumaini watazika kesho (leo) kwa sababu hata kaburi haijachimbwa, nitajitahidi kuhudhuria maziko,” alisema diwani huyo.

Kifo cha Nurdin kinafanya idadi ya watu waliouawa katika eneo hilo kufikia zaidi ya 30.

Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amefika eneo hilo na kuzungumza na askari ambao wanaendesha msako mkali usiku na mchana.

 Mauaji ya viongozi wa kisiasa na Serikali yanayoendelea Kibiti yanaonekana kuumiza vichwa vya wengi kutokana na polisi kuyahusisha na vitendo vya ujambazi, huku Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kikisema yana harufu ya kigaidi na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, akikinzana na mitazamo hiyo.

Rekodi zinaonyesha Mei 13, mwaka huu, Katibu wa CCM Kata ya Bungu, Wilaya ya Kibiti, Halife Mtulia, alipigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana alipokuwa akitoka uani.

Aprili 14 mwaka huu, askari polisi wanane waliuawa na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi katika Kijiji cha Makengeni wilayani Kibiti.

Januari 19, mwaka huu, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Nyambunda, Oswald Mrope, aliuawa baada ya kupigwa risasi mbele ya familia yake. 

Februari 3, mwaka huu, watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto, huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuwatoroka. 
Februari 21, mwaka huu, watu watatu akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi. 
Machi Mosi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana, aliuawa.

Aprili 29, mwaka huu, mkazi wa Kijiji cha Mgomba Kaskazini, Kata ya Mgomba, Ikwiriri, Hamad Malinda, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.  

Mei 5, mwaka huu, kada wa CCM Wilaya ya Rufiji, Amir Chanjale, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. 
Oktoba 24, 2016, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda, Ally Milandu alipigwa risasi na kufariki na Novemba 6, 2016, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyang’unda, Kijiji cha Nyambunda, Mohammed Thabiti, alipigwa risasi akielekea kwake. 

Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa mkaguzi wa kituo cha ukusanyaji mapato ya ushuru Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi mgambo. 
Katibu wa CCM Wilaya ya Kibiti, Zena Mgaya, alikaririwa na vyombo vya habari akisema Kijiji cha Nyambunda, Kata ya Bungu kimepoteza mwenyekiti, mtendaji na wenyeviti watatu wa vitongoji vilivyoko katika kijiji hicho. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles