TEHRAN, IRAN
HATIMAYE Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran imemtangaza Hassan Rouhani kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa rais kwa kumshinda mpinzani wake mwenye msimamo mkali, Ebrahim Rais.
Wizara hiyo imemtangaza Rouhani kuwa mshindi wa uchaguzi huo baada ya kujizolea zaidi ya kura milioni 22 dhidi ya zaidi ya milioni 15.
Rouhani, mwenye umri wa miaka 68, mwanamageuzi aliyeiongoza nchi yake kufikia makubaliano ya kihistoria na nchi sita zenye nguvu zaidi duniani kuhusu mpango wake wa kinyuklia, ameshinda uchaguzi huo uliofanyika hapo jana kwa asilimia 57 ya kura.
Amemshinda mpinzani wake mkuu, Ebrahim Raisi, ambaye alikuwa anaungwa mkono na baraza lenye ushawishi mkubwa la masheikh wa Kiislamu wasiochaguliwa kupitia chaguzi.
Uchaguzi huo umetajwa kama kura ya maoni ya kupima utendaji wa Rouhani kuhusu juhudi zake za kuifungulia fursa nchi yake kwa mataifa ya magharibi. Kituo cha televisheni cha Iran kimempongeza Rouhani kwa ushindi huo unaombakisha madarakani.