Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM
TIMU ya taifa ya vijana walio chini ya miaka 17, Serengeti Boys, leo inarusha karata yake muhimu dhidi ya Niger katika mchezo wa Kombe la Afrika kwa vijana nchini Gabon.
Mchezo huo utafanyika katika Uwanja wa Port Gentil mjini Port Gentil, ambapo kikosi hicho kikiwa kimevuna poibnti nne katika michezo yake miwili ya awali, ikianza kupata suluhu dhidi ya Mali Mei 15, mwaka huu kabla ya kuifunga Angola mabao 2-1.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime amesema kuwa mchezo huo ni muhimu kupata matokeo ili kujiweka katika nafasi ya kucheza hatua inayofuata.
“Tumejiandaa vema kuwania nafasi ya angalau kuingia nusu fainali,” alisema Shime.
Naye Nahodha wa timu hiyo, Dickson Job aliwatoa shaka Watanzania akisema vijana wote wako vema kwa ajili ya mchezo huo kwani mpira wa miguu kwao ni ajira kwa manufaa ya yao binafsi, familia na taifa ambalo limewatua Gabon kutafuta Kombe la Mataifa ya Afrika.
Serengeti Boys inahitaji sare ya aina yoyote ili iweze kuvuka huku Niger ambayo ina pointi moja ikiburuza mkia katika Kundi B.