26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

MBAO YATIA DOA UBINGWA YANGA

Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia ubingwa baada ya kukabidhiwa kombe katika Uwan ja wa CCM Kirumba, Mwanza jana. PICHA na LODRICK NGOWI

 

MWANDISHI WETU- MWANZA na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

TIMU ya Yanga ilikabidhiwa rasmi ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2016/17 licha ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbao katika mchezo wa mwisho uliochezwa jana Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Yanga imetawazwa rasmi kuwa mabingwa wa ligi hiyo kwa mara ya 27 baada ya kufikisha pointi 68 sawa na wapinzani wao wa karibu Simba ambao hata hivyo walizidiwa kwa tofauti ya idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mashabiki wa Yanga licha ya kupoteza mchezo huo, walionekana wakishangilia kwa shangwe ubingwa huo baada ya Nadir Haroub ‘Canavarro’ kukabidhiwa kombe.

Katika mchezo huo, bao la Mbao lilifungwa na Habibu Haji katika dakika 22 na kuiwezesha timu hiyo kusalia Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao.

Matokeo hayo yameiwezesha Mbao kufikisha pointi 33 huku ikiziacha timu za JKT Ruvu ya mkoani Pwani, Toto African ya Mwanza na African Lyon zikitupwa nje ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

African Lyon ambao walihitaji ushindi kuepuka kushuka daraja walilazimishwa sare ya kutofungana na Tanzania Prisons mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya hivyo kubaki na pointi zao 32.

Toto Africans walipoteza mchezo wao wa mwisho 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turuiani mkoani Morogoro na kubaki ka pointi zao 29 ambazo hazingewawezesha kuepuka kushuka daraja.

JKT Ruvu ambao ndiyo ilikua timu ya kwanza kushuka daraja ikiwa na pointi zake 23 ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka Ndanda FC.

Ushindi wa Ndanda FC dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, uliwawezesha kubaki kwenye Ligi Kuu Bara licha ya wadau wengi wa soka kuitabiria mwisho wao umefika.

Wakati Yanga wakikabidhiwa ubingwa, watani wao wa jadi timu ya Simba wao wameifunga Mwadui mabao 2-1 katika mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba walianza mchezo huo kwa kasi uliochezeshwa na mwamuzi Erick Onoka kutoka Tanga, huku wakioneka kuhitaji ushindi mapema.

Kasi hiyo iliiwezesha Simba kupata bao la kwanza dakika ya 17, lililofungwa na mshambuliaji Shiza Kichuya kwa mkwaju wa penalti.

Kuingia kwa bao hilo kuliongeza kasi na Simba kujipatia bao la pili katika dakika ya 24 lililofungwa na Ibrahim Ajibu, baada ya kupokea krosi kutoka kwa Juma Luizio.

Licha ya mabao hayo, Mwadu ilikuja juu na kufanikiwa kupata bao la kufuta machozi dakika ya 43, lililofungwa na Paul Nonga baada ya kupokea krosi ya Salum Kabunda.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko kwa kumtoa Juma Luizio na kuingia Said Ndemla.

Katika dakika 60 Mwadui walifanya mabadiliko kwa kumtoa Salim Kabunda na kuingia Abdallaah Seseme.

Mwadui pamoja na kufanya mashambulizi langoni mwa Simba walijikuta wakitoka uwanjani kwa kufungwa mabao 2-1.

Simba imefikisha pointi 68 na kushika nafasi ya pili, ambazo Yanga pia imevuna pointi hizo 68 lakini ikiwa na wastani mzuri wa mabao ya kushinda na kufungwa.

Katika michezo mingine ya ligi hiyo, Azam FC wamekubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar.

Matokeo hayo yameiwezesha Kagera Sugar inayonolewa na kocha Mecky Mexime kufikisha pointi 53 na kushika nafasi ya tatu.

Majimaji imeifunga Mbeya City mabao 2-1 katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea huku Stand United ikiifunga Ruvu Shooting bao 1-0.

Simba:

Daniel Agyei, Javier Bukungu, Mohammed Hussein, James Kotei, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzammiru Yasin, Laudit Mavugo, Ibrahim Ajibu, Juma Luizio

Mwadui:

Shaaban Kado, David Luhende, Abdallah Mfuko, Nassoro Hemed, Joram Mgeveke, Razack Khalfan, Awadhi Juma, Miraji Athuman, Salim Kabunda, Hassan Kabunda, Paul Nonga

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles