25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

AJIRA ZISIZORUHUSIWA KWA MTOTO KISHERIA

Kisheria hairuhusiwi watoto kusimamia harusi

 

Na Christian Bwaya,

MARA nyingi tumeshuhudia picha za watoto waliodhalilishwa kijinsia zikisambazwa na watu wazima kupitia mitandao ya kijamii. Teknolojia imefanya iwe rahisi watu kupata taarifa na kuzieneza wakati mwingine bila kutafakari madhara ya kufanya hivyo.

Pengine inawezekana, wakati mwingine, mstuko wa kuona taarifa isiyo ya kawaida humsukuma mtu kusambaza taarifa anayoipata bila kuchukua tahadhari. Siku chache zilizopita, niliona picha za mtoto mdogo anayedaiwa kubakwa zikisambazwa mitandaoni.

Huu ni mfano wa vitendo tunavyovichukulia kirahisi lakini vinavyoweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto. Pamoja na uchungu wanaokuwa nao watu wanaosambaza picha hizo, ni vigumu kuelewa kama kweli wanatafakari athari za sasa na baadae kwa mtoto mwathirika. Fikiria mtoto atakavyosikia pale atakapokuwa mtu mzima mwenye marafiki, anapoona picha zinazoonesha sura yake zikipatikana mtandaoni.

Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009 imeainisha baadhi ya vitendo vilivyozoeleka katika jamii na wakati mwingine vikichukuliwa desturi, lakini visivyojali hisia na haki za mtoto. Hapa tunavitaja vichache.

Tohara ya mtoto wa kike

Serikali, kwa ushirikiano wa mashirika mbalimbali, imefanya jitihada za kutokomeza tohara ya mtoto wa kike. Pamoja na kupungua, bado zipo jamii zinazoendeleza mila hii potofu inayosababisha matatizo mengi kwa mtoto hasa anapokuwa mtu mzima. Sheria hii imefanya ukeketaji uwe kosa kisheria.

Picha na habari zinazomdhalilisha mtoto

Katika kulinda heshima ya mtoto, sheria hii kadhalika imefanya iwe kosa kwa mtu yeyote kuchapisha, kuzalisha, kuonesha au hata kusaidia kuchapishwa, kuzalishwa au kuoneshwa kwa picha ya mtoto mzima au maiti yake yenye majeraha ya kudhalilishwa au mkao wa kingono. Ndio kusema kitendo cha baadhi ya watu au vyombo vya habari kuonesha picha za watoto wahanga wa matukio ya udhalilishaji au unyanyasaji ni kinyume cha sheria. Kadhalika, kwa mujibu wa sheria hii, ni kosa kuchapisha au kusaidia kuchapishwa kwa taarifa zenye mrengo wa kumnyima mtoto haki yake.

Kubadili dini ya mtoto

Tunafahamu vipo vituo vinavyopokea watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ambavyo mbali na kuwapa huduma huwashinikiza kubadili dini. Sheria hii imezuia kitendo hicho na kufanya iwe kosa kisheria kuwalazimisha watoto kubadili dini waliyozaliwa nayo.

Kutumia vibaya misaada

Katika siku za hivi karibuni kumekuwapo taarifa za miradi inayojinasibu kumtafutia mtoto misaada ikitumika kwa maslahi ya watu binafsi. Watoto wamekuwa wakitumika kama daraja la kuhalalisha upatikanaji wa misaada inayoishia kwenye matumbo ya watu binafsi.

Sheria hii imelitambua hilo. Imefanya kitendo cha mtu yeyote au taasisi kutumia vibaya misaada ya aina yoyote iliyolengwa kumnufaisha mtoto kuwa kosa kisheria. Lengo ni kuhakikisha kuwa haki anazostahili mtoto zinalindwa.

Kumtumia mtoto kwenye urembo

Habari za watoto kutumiwa kama mapambo ya harusi si ngeni katika jamii zetu. Maharusi wengi huandaa watoto wadogo kama ‘maharusi wadogo’ kwa lengo la kupendezesha harusi yao.

Hata hivyo, wakati mwingine shughuli hizi huendelea mpaka usiku wa manane. Watoto wanaokaa kama mahurusi huchoka kiakili na kimwili. Mbali na kumchosha mtoto, shughuli hizi pia hupenyeza mawazo yasiyolingana na uelewa wa watoto. 

Sheria ya mtoto imefanya iwe kosa kwa mtu yeyote kumtumia mtoto kama mapambo ya harusi, maonesho ya mitindo au shughuli nyingine zinazofanana na hizo zinazofanyika usiku.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles